Harmonize Akiachwa na Sarah Atarudi Kupiga Goti WCB



UBISHI wa leo kijiweni hauna muhtasari. Jionee mwenyewe Luqman Maloto na Dk Levy walivyoleteana ‘vagi’ la maneno.

LUQMAN: Unadhani Ali Kiba na Hamisa Mobetto wapo Zanzibar hoteli moja wanafanza nini hasa?

DK LEVY: Ali Kiba ni msusi mzuri sana wa nywele na ukili. Sasa pengine anamfundisha ususi. Na pia pengine ndo wapo kwenye karantini yao waliyochagua.

LUQMAN: Hivi ninyi Konde Gang si mmeoa Italia? Mnapiga simu kweli kujua ukweni kwenu kinachoendelea na Corona?

DK LEVY: Kwa faida yako. Italia siyo taifa la watu wa kutegemea msaada wa wakwe kwenye matatizo. Usichanganye aina ya maisha ya kina Tanasha na Amina hapo Kenya pamoja na Zari, Uganda. Yule wa Konde Boy familia yake ina bima ya maisha. Matatizo yao yanajitatua kwa bima siyo kelele za mawifi. Usituletee uswahili wa Madale.

LUQMAN: Kwa hiyo kama wana bima ndio hata kujuliana hali hairuhusiwi? Au na hilo la kuulizana hali linalipwa na bima?

DK LEVY: Jifunze tamaduni za Wazungu kwanza kabla ya kuanza kubwabwaja hapa. Wale ndo Warumi. Watawala wa Israel ya kale enzi za Pontio Pilato. Hata tukiwasiliana na ukweni sio lazima nyie makorona mjue. Yaani zile swaga za Madale kutaka kuonesha kila kitu hadharani tuliwaachia wenyewe. Vitu vinaenda chini kwa chini kama mizizi ya mbuyu. Upo nyonyo?

LUQMAN: Nyonyo mwenyewe, usiniletee vimisemo vya kishirikina hapa. Haya ninyi Konde Gang ndio mmeoa peponi na Sarah ni mwanamke wa peponi. Maisha mmeshayapatia mpaka mwisho. Badala ya kujisifia kazi kama WCB, ninyi sifa mnampa Sarah. Inaonekana bila Sarah Konde Gang haipo. Na kama Sarah angekuwa hatoki Italia sijui ingekuwaje? Mwanaume kukaa kila siku unasifia uzuri wa ukweni ni uzwazwa. Fanyeni kazi muweze kujisimamia wenyewe kama Diamond na WCB, sio sasa hivi, Sarah akichomoa shilingi lazima mrudi WCB kuomba msamaha.

DK LEVY: Sikutegemea kama unaumizwa na Konde Gang kwa kiwango hiki. Nitakupa albamu ya AfroEast bure kabisa. Naamini ukisikiliza ngoma mbili tu utaelewa kwa nini Konde Boy yuko nje ya WCB. Moja kati ya slogan kibao za Konde Gang ni hii ya “Fanya Maisha Kitu Kitamu Ufurahie.” Naona una maneno mengi. Njoo upewe mchongo Konde Gang, tunahitaji watu wenye maneno mengi kwa ajili ya kujibishana na mashabiki mitandaoni.

LUQMAN: Konde Gang kwa sasa ni kama Barcelona, bila Messi hakuna kitu. Pale Konde Gang, Messi ni Sarah. Yeye ndiye anafanya ile taasisi iwepo. Mfano Sarah akiamua kurudi Italia kwao, ninyi Konde Gang mtaambia nini watu? Mtapata wapi pesa za kukodi ukumbi Mlimani City? Nani atawalipia pesa ya kukodi helikopta kwenda nayo Tandahimba? Nani atawalipia deni milioni 500 WCB?

DK LEVY: Umenikumbusha mbali. Kuna wakati mataifa ya nje yalisema Tanzania hakuna amani ila Nyerere ndo anawabana. Siku akiondoka hatutaelewana. Kiko wapi? Na kuna watu walisema bila Ruge Clouds hamna kitu. Kiko wapi? Na wapo waliosema bila Manji Yanga hamna kitu. Kiko wapi? Pia mlisema bila Zahera. Sasa mtaanza kusema bila Morrison. Konde Gang ni taifa ndani ya taifa. Sisi mameneja wetu siyo wapiga dufu ni wasomi watupu.

LUQMAN: Sasa nani mameneja wao ni wapiga dufu? Acha dharau wewe. Unataka kusema nani, Sallam, Tale au Fella? Wale wote wana viwango vyao. CV zao kwenye muziki ni heavyweight. Sio hao mameneja wenu, kuna madaktari, badala ya kwenda kutibu wagonjwa wao wanakomaa kupiga deiwaka kwa Harmonize. Sasa Sarah akiacha kulipa posho itakuwaje?

DK LEVY: Tofautisha mameneja na wasaidizi. Hao wa WCB ni wasaidizi wa shughuli za Mondi. Sallam kuagizwa kutafuta na kupokea simu za wasanii na mapromota wa nje. Tale kazi yake kusimamia vishughuli vya ndani ya nchi. Kama misiba, harusi, vikao na watu. Na zaidi kuhakikisha familia za Mondi zinapelekewa mahitaji muhimu. Fella michongo yake kuangalia njia mbadala za kuzuia kesi ngumu, kuzuia mvua kwenye matamasha ya WCB. Kutafuta watu wa albadil, kisomo na duwaa kwa wasanii wa WCB. Yaani Mondi ndo msanii anayefanya kazi ya ‘kumeneji’ mameneja wake.

LUQMAN: Kwanza Fella ni diwani. Yaani Diamond ana meneja ambaye ni kingozi mwenye kiapo. Mjumbe wa halmashauri. Sasa ninyi kwenu Konde Gang mna meneja diwani? Mna meneja kama Sallam? Mnamfikia Tale? Konde Gang Sarah ndiye mmiliki wa hisa asilimia 100. Mna chenu hapo?

DK LEVY: WCB mmiliki mkuu ni mama kifaa cha Big Joo, na huku mnataka awe mwanamama? Sawa ni Sarah mwenye asilimia 100. Lakini unafahamu kuwa ndoa ni mwili mmoja? Sasa huko kwenu mwenye hisa nyingi sio mwili mmoja na Mondi Laden. Kwa hiyo acha kujifananisha wanandoa na wanahisa. Ni kwamba Msimbazi tunataka kumleta Okwi tena na Yondani. Ili tushindane na Mazembe, Al Ahly, Zamalek na mitimu yote mikubwa kubwa. Ila kitu Cha kwanza ni kumdondosha Okwi hapa ‘suuni azi posibo’.

LUQMAN: jibu swali; Bosi mkuu wa Konde Gang, Sarah, akisema hataki tena biashara ya muziki, vipi mtarudi WCB kuomba nafasi? Au mtaenda Kings Music kwa Ali Kiba?

DK LEVY: Kinachofurahisha mnazijua sana taarifa za Sarah kuliko za Zari. Hivi Tiffah anajua Kiswahili kweli? Sisi Maanko lazima tufahamishwe. Haya mambo ya kukutana nako na kuanza kusema Tototooo, Chuchuchuuu ajigijigijiiii. Kanaweza kuita polisi kakidhani tunakaambukiza corona kwa njia ya lugha isiyoeleweka. Lazima watoto wajue lugha ya nyumbani. Lakini mpaka sasa sioni dalili. Tusije kuwa tumekaa kama matofali huku tunaamini tuna familia ‘Sauzi Afrika’. Kumbe kakabidhiwa Awilo Longomba au Julius Malema.

LUQMAN: Kwani mkishajua kama Tiffah hajui Kiswahili ndio hisa za Konde Gang zitahama kutoka kwa Sarah na kwenda Harmonize? Acha maswali yasiyo na tija. Tuache hilo, tujadili mambo ya afya timamu. Mbona kocha wa Yanga anambania Yikpe? Unajua yule ni bonge la straika, sasa mbona hapangwi? Kocha Luc anahujumu timu kwa kumweka benchi muuaji Yikpe.

DK LEVY: Kama unataka tija anza kuongelea mchezaji mzawa Ajibu anayebaniwa pale Simba. Yule akipewa nafasi ataisaidia na Stars pia. Sasa unaongelea mtu kutoka Ivory Coast wa nini? Na habari za ndani ni kwamba hata kikosini kaondolewa hivi sasa anacheza marede na Simba B.

LUQMAN: Mbona umekuwa mkali kumsema Yikpe? Haya tuyaache hayo, ngoja nikuulize swali tofauti; Kwa nini mashabiki wa Yanga hampendi kusikia jina la Yikpe? Kawafanya nini?

DK LEVY: Kwa sababu anajua sana kiasi kwamba wazawa wanakosa nafasi. Sasa mashabiki wa Yanga Hilo linawakera kuona ufundi wake mtu mgeni unamnyima nafasi Ngassa, Kaseke, na Tariq Seif. Unamuongelea sana Yikpe unataka kumsajili? Kwa faida ya Taifa Stars tuulize akina Rashid Juma, Muzamiru, Ajibu, Kichuya na wenzao.

LUQMAN: Ile ni timu ya kimataifa, ina kikosi kipana. Kila mchezaji ni kifaa. Wote uliowataja, Yanga wanaanza kikosi cha kwanza. Mna hela ya kuwanunua?

DK LEVY: Waitwe kwanza timu ya taifa ndo watafikiriwa kucheza na Morrison. Yanga siyo jalala wala karantini la kuhifadhi makorona ya mpira.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad