Hatimaye Malalamiko ya Marefa Kuboronga Ligi Kuu yatua Serikalini
0
March 03, 2020
KUFUATIA kuwapo kwa sintofahamu ya uwezo wa waamuzi wanaochezesha mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo sasa iko katika hatua ya lala salama, serikali imesema imepokea rasmi malalamiko kutoka kwa wadau wa mchezo huo hapa nchini.
Akizungumza jana jijini hapa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbas amesema wadau hao wanalalamika kuwapo kwa upendeleo katika baadhi ya michezo unaofanywa na waamuzi ambao wamepewa dhamana ya kuchezesha.
Abbas alisema malalamiko mengine ni kuwapo tuhuma za upangaji wa matokeo na madai ya rushwa katika baadhi ya mechi na ili kumaliza tatizo hilo, ofisi yake imeliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kufuatilia na kuchunguza kwa kina malalamiko hayo.
Kiongozi huyo alisema ofisi yake inataka kuona malalamiko na kero hizo zinafanyiwa kazi haraka.
“Naamini wiki ijayo (wiki) nitaonana nao (BMT), na kuangalia nini kinaendelea,” alisema Abbas.
Sambamba na hilo, alivitaka vyama vya michezo nchini kuwa na utawala bora katika utendaji kazi wao.
“Tunataka utawala bora kwenye vyama vya michezo kama soka, TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), ihakikishe kwamba kuna utawala bora zipo kamati sijui za saa 24 zifanye kazi,” alisema.
Katibu Mkuu huyo pia alimwagiza Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo, kuhakikisha kila chama kinakuwa na bajeti ili kujua kiasi cha fedha ambacho inapata kwa kila mwaka.
“Baadhi ya vyama vimekuwa vikipokea ruzuku pamoja na kukusanya tozo na michango mbalimbali, lakini linapokuja suala ya timu ya Taifa huanza kutembeza bakuli la kuomba kwa serikali, pia tupate ratiba ya vyama vyote, umekaa ofisini ghafla anaibuka kiongozi wa timu ya vinyago inaenda sijui wapi, mmekaa kidogo kuna mashindano ya rede Pakstani,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo alisema anaamini mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga utakaochezwa Jumapili utakuwa mzuri na kuahidi atakuwapo uwanjani kushuhudia mechi hiyo.
Tags