Raia Wakigeni Wakubwa na Hofu ya Kunyanyapaliwa Kisa Corona




Huku maambukizi ya Corona yakiendelea kuongezeka Afrika, hofu ya janga hili linalokumba dunia imesababisha ubaguzi dhidi ya raia wa kigeni Afrika Mashariki.

Kutoka Ethiopia kuelekea Kenya na hadi Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, raia wa kigeni wamekuwa wakishambuliwa kwa maneno ma hata kupigwa kwasababu ya hofu ya kwamba huenda wameambukizwa virusi vya Covid 19.

Hii ni kwa sababu visa vingi vilivyoripotiwa katika eneo hilo vinadaiwa kuletwa na wageni waliowasili kutoka mataifa ya Ulaya na Marekani

Mwandishi wa BBC, Emmanuel Igunza ametembelea mji wa Iten na kukutana na baadhi ya wanariadha wa kigeni.

Mji wa Iten magharibi mwa Kenya unafahamika kote duniani kama kitovu cha mabingwa wa Olimpiki na mabingwa wa dunia katika riadha.

Ni kaya kwa wanariadha wengi ambao wanashikilia rekodi ya dunia kuliko sehemu nyengine yoyote duniani.

Kwahiyo ni jambo la kawaida kuona kwamba wanariadha wengi wa kimataifa duniani wamesafiri na kufanya mji huu kuwa eneo lao la kufanyia mazoezi.

Lakini katika wiki za hivi karibuni wanariadha wa kimataifa wamekuwa wakishambuliwa na wenyeji ambao wanawashutumu kuwa wameambukizwa virusi vya Corona.

Kocha wa Uhispania Totti Corbalan ni miongoni mwa waliokutana na mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza .

''Ni watu ambao wanatuambia kuwa sisi tumeambukizwa virusi vya Corona kwahiyo watoto na watu wazima wanapotuona, wanafikiria kwamba sisi ndio wenye virusi vya corona na hapo hapo wanaanza kutukimbia na kutucheka.

Kocha wa Uhispania Totti Corbalan alikuwa wa kwanza kutangaza hadharani unyanyasaji huo baada ya kupigwa mawe na kuitwa "corona" wakati anafanya mazoezi katika mji huo.

''Siku moja nilipokuwa nikikimbia pekee yangu, kundi moja la watoto lilikuwa limejificha nyuma ya mti na ghafla nilipokuwa nikiwapita, walianza kujaribu kunirushia mawe lakini niliwagundua mapema kwani wakati huu niko chonjo kujua kinachotokea eneo niliko. Kwa hiyo nilikwenda hadi walikokuwa na nikawaelezea kwamba wanachofanya sio sawa. Niliwauliza ni kwa nini wananitupia mawe? Ni kwa nini wananiita Corona?

Takriban wanariadha wanne wameiambia BBC kwamba wamewahi kupitia madhila kama hayo. Mwanariadha wa Uswizi Alex Jodidio ambaye anafanya mazoezi yake katika mji huo anasema ameshuhudia tabia za watu kubadilika tangu ilipotangazwa kuwa Ulaya ndio kitovu cha janga la Corona.

Alex Jodidio anasema, '' Nimeona mabadiliko madogo kwani nimekuja hapa Iten mara nyingi sana. Pia nina marafiki kadhaa ambao sasa wananiogopa labda kwa sababu mimi ni mzungu na hali ya sasa ya bara Uropa ni tete. Kwa hiyo nahisi tofauti. Nimeitwa Corona katika mitaa na kuna baadhi ya watu ambao nawajua wamejitenga lakini naheshimu kila Mkenya kwani natambua kuwa labda wana hofu. Lakini nadhani hii ni kwa muda tuu na mambo yatakuwa bora zaidi hivi karibuni.''

Baadhi ya wanariadha wa kimataifa wanaofanya mazoezi katika mji wa Iten kwa sasa wanapendelea kutoka wakiwa kama kundi na wakiwa pamoja na wanariadha wenyeji ili kuepuka kushambuliwa.

Wakatihuohuo, wanariadha mashuhuri wa eneo hilo wamelaani vikali mashambulio hayo dhidi ya wakimbiaji wa kigeni.

Lakini visa hivi havijatokea tu nchini kenya. Katika maeneo mbalimbali mashariki mwa Afrika, raia wa kigeni wameripoti kwamba wamekuwa wakishambuliwa kwa hofu ya virusi vya Corona ambavyo pia vinafahamika kama Covid 19.

Mwezi uliopita, Waziri Mkuu wa Ethiopia ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel, Abiy Ahmed, alitoa wito kwa raia wa Ethiopia wasishambulie raia wa kigeni baada ya ubalozi wa Marekani kutoa tahadhari kwa raia wake wanoishi nchini humo baada ya raia wa kigeni kushambuliwa kwa kurushiwa mawe, kufukuzwa na kutemewa mate, huku hofu ya ugonjwa wa Corona ukiendelea kusambaa kote duniani.

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mfanyakazi mmoja wa shirika la kutoa msaada ambaye hakutaka kutambulishwa, ameiambia BBC kwamba raia wa kigeni wanaofanyakazi katika mashirika ya kutoa misaada wamelazimika kuangalia tena usalama wao baada ya misafara kadhaa ya kutoa misaada ya binadamu kurushiwa mawe. Baadhi yao pia wameshambuliwa kwa kurushiwa maneno machafu na kuitwa coronavirus mitaani.

Mfanyakazi huyo amesema: ''Iwapo mashambulio kama haya yataendelea, huenda shughuli zetu za kutoa misaada zikaathirika pakubwa. Hii sio tofauti na kama vile kwa mfano, makundi yaliyojihami kushambulia mashirika yasiyokuwa ya kiserikali. Hii italazimu kuchunguza upya taratibu zetu za usalama. Haya ni masuala ambayo lazima tutatilia maanani.''

Hofu imesababisha ubaguzi hata katika mitandao ya kijamii na serikali mbalimbali zimejitahidi kukabilinana na taarifa ghushi za Coronavirus. Lakini katika mji wa Iten, mwanariadha wa Uswizi Alex Jodido ana ujumbe maalum wa umoja katika kile anachokielezea kama wakati mgumu kote duniani... ''Nadhani ni jambo la kusikitisha sana lakini nawaelewa Wakenya kwa sababu ya hali ilivyo. Lakini nahisi kuwa watulivu….hakuna matata, ni lazima tuwe pamoja wakati huu.''

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad