Huyu Hapa Aliyemleta Morrison Bongo



KIUNGO Mshambulizi nyota wa Yanga, Bernard Morrison, amekuwa gumzo katika soka nchini baada ya kujiunga na timu hiyo akitokea kwao Ghana ingawa swali kubwa limekuwa ni hivi; nani aliyemuona na kumleta Yanga?

Wakati Morrison amesajiliwa Yanga, baada ya mashabiki wasio wa Yanga kupata taarifa alikuwa akicheza Orlando Pirates ya Afrika Kusini, walianza kumbeza kwamba kama alikuwa bora asingeachwa huko.

 

Baada ya kutua nchini na kuanza kufanya vizuri, gumzo likawa ni nani aliyemleta kwani hata Simba nao wakaanza kufanya njia za kuhakikisha wanataka kumsajili lakini wakakwama mwishoni. Yeye Morrison amefanya mahojiano maalum na kueleza siri ya yupi hasa aliyemleta nchini.
“Nilipata ofa nyingi sana wakati nikiwa nyumbani Ghana, timu mbalimbali za barani Afrika zilitaka niende na kujiunga nazo na wakati fulani timu za Afrika Kusini ndio zilionyesha nia sana.
“Pamoja na hivyo, kocha (Luc Eymael wa Yanga), alikuwa kati ya niliokuwa nao karibu na mara nyingi alinisisitiza kujiunga naye. Kweli alikuwa ni mtu aliyewasiliana nami mara kwa mara ikiwepo kunipa ushauri.
“Mwanzo nikakubali kurejea Afrika Kusini kujiunga na timu yake, wakati nikiwa katika maandalizi ya mwisho, kocha Eymael akanipigia simu na kunieleza kwamba haitakuwa Afrika Kusini tena badala yake Tanzania ambako amepata timu inaitwa Yanga.
“Kwa kuwa nilishakubaliana naye, sikuwa na namna nikasema nitakwenda Tanzania kufanya kazi. Bahati nzuri nilipata mapokezi mazuri sana na ninamshukuru mtu kama Injinia Hersi, nilipofika nilizungumza naye sana na kupata matumaini kuwa hapa ni sehemu nzuri ya kufanyia kazi,” anaelezea Morrison.

Tayari Morrison ni mchezaji gumzo zaidi kwa mashabiki wa soka nchini kwa upande wa Yanga na amekuwa kivutio kutokana na vituko vyake vingi uwanjani lakini uwezo mkubwa wa kuwatoka mabeki, kupiga pasi nzuri na kufunga ndio umempa umaarufu mkubwa.

Kabla ya kuichezea Yanga, Morrison alikaa kwa mwaka mzima bila ya kucheza soka la ushindani lakini kabla ya hapo aliitumikia Orlando Pirates ya Afrika Kusini pia AS Vita ya DR Congo akiwa mmoja wa wachezaji wanaotegemewa katika vikosi hivyo kongwe na vikubwa barani Afrika.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad