KESI ya mauaji namba 131 ya mwaka 2017 inayomkabili mfanyabiashara na mmiliki wa mabasi, Jumanne Wang’anyi, maarufu kama J4, mkazi wa Nyakato jijini Mwanza, imeanza kusikilizwa na kutolewa ushahidi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza.
Kesi hiyo ilianza kusikiliza Machi 3, 2020 mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Sam Rumanyika, Upande wa Mashtaka ukiongozwa na Wakili Robert Kidando na Upande wa Utetezi unaongozwa na Wakili Anthony Nasmir.
Mbele ya Jaji Rumanyika, shahidi wa kwanza, Donatha Gabriel, ambaye ni mke wa marehemu Ally Abeid, na shahidi wa pili, Aziza Sekarwanda, ambaye ni dada wa marehemu Cloud Sekarwanda, walidai mahakamani kuwa mnamo Julai 13, 2015 ambayo ni siku ya tukio hilo la mauaji, waliagwa na Abeid na Sekarwanda (wote marehemu) kuwa wanakwenda kuonana na bosi wao ambaye ni mfanyabiashara huyo.
Inspekta Benidict Manyanda ambaye ni shahidi wa tatu katika kesi hiyo, alidai mahakamani kuwa siku ya tukio, alifika eneo la tukio na kukuta miili ya watu wawili ikiwa chini na baadaye kuipelekea hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Akitoa ushahidi wa tukio hilo, shahidi wa nne, Inspekta wa Polisi Masaga Francis kutoka Kitengo cha Uhalifu kwa Njia ya Mtandao, alidai mahakamani hapo kuwapo kwa mawasiliano ya kimtandao baina ya marehemu Abeid na mshtakiwa J4 kuanzia Mei 2015 hadi Julai mwaka huo na hata siku ya siku hiyo ya tukio.
Mfanyabiashara huyo anadaiwa kuwa Julai 13, 2015, aliwaua kwa kuwapiga risasi wafanyabiashara wanzake wawili; Ally Abeid na Cloud Sekarwanda, eneo la Nyakato Boma lililoko sehemu ya kuhifadhi magari ya kampuni ya mshtakiwa huyo.
Jaji Sam Rumanyika aliahirisha kesi hiyo hadi kesho itakapotajwa tena huku mtuhumiwa akirudishwa mahabusi kwenye Gereza Kuu la Butimba jijini.