WAKATI uongozi wa Yanga kwa kushirikiana na wadhamini wao, Kampuni ya GSM, wakiendelea kuboresha mikataba inayoelekea ukingoni kwa nyota waliopendekezwa na kocha Luc Eymael, kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ bado ana mkataba wa muda mrefu.
Feisal ni mmoja wa wachezaji ambaye iliripotiwa kuwa mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Injinia Hersi Said ambaye ni Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM lakini pia akiwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, amesema mkataba wa Feisal bado haujamalizika na hata kama ungekuwa unamalizika wasingekubali kumuachia.
Aidha, Hersi amewahakikishia wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa wamejipanga kujenga kikosi imara, hivyo hawatakuwa na masihara kwenye usajili wa nyota watakaoitumikia Yanga msimu ujao.
“Wanayanga waondoe hofu, Feisal anabaki Yanga haendi popote pale mkataba wake ukimalizika tutamuongezea mwingine,” alisema Hersi.
Imeelezwa Feisal alisaini mkataba wa miaka mitatu wakati akijiunga na Yanga mwaka 2018, hivyo mkataba wake utamalizika mwaka 2021.