Kocha Yanga Aruhusu Udambwi wa Morrison




KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael, amefunguka kuwa kitendo cha kumkataza kiungo wa timu hiyo, Bernard Morrison raia wa Ghana kutembea juu ya mpira kilimletea shida kutoka kwa mashabiki hali iliyomfanya aruhusu kuendelea kufanywa kwa sharti la kuwaheshimu wapinzani wao.

 

Mbelgiji huyo ametoa kauli hiyo kufuatia ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo dhidi ya Alliance ambapo Morrison alionyesha staili nyingine ya shibobo kabla beki wa kushoto wa timu hiyo, Jaffar Mohammed hajaulalia mpira kwa kifua mbele ya mchezaji wa Alliance.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Eymael alisema kuwa ameamua kuruhusu wachezaji kuendeleza staili hiyo ya kucheza mpira kwa kuwa imekuwa ikipendwa na mashabiki huku akisisitiza suala la kuendelea kuheshimu wapinzani wao.

 

“Mpira ni mchezo ambao unaenda na burudani siku zote ndiyo wanachokifuata mashabiki, siyo kwamba natetea kilichofanyika kwa sababu sipendi kuona shibobo ikitumika zaidi kwani huleta mambo magumu pia inaonyesha hakuna heshima kwa mpinzani.

 

“Lakini naona niache waendelee kutumia shibobo kwa sababu mashabiki wanapenda kuona hivyo na iliniletea shida nilivyomkataza Morrison alipofanya wakati ule, ‘leo’ imetumika na mashabiki wamefurahi ila zaidi wafanye kwa kuheshimu wapinzani na siyo kuwadharau,” alisema Eymael.

LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad