Lipumba atoa Ufafanuzi juu ya Ripoti ya CAG



SIKU moja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kukabidhi ripoti ya ukaguzi wake ya 2018/19 kwa Rais John Magufuli , Chama cha Wananchi( CUF) kimeamua kujitetea baada ya ripoti hiyo kubaibainisha Chama hicho kilihamisha kwa fedha kutoka akaunti ya Chama hicho kwenda akaunti binafsi. 

Akizungumza leo Machi 27,2020 ,Mwenyekiti wa Chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba ametumia nafasi hiyo kuwaeleza waandishi wa habari hatua kwa hatua kuhusu fedha hizo ili kuweka Kumbukumbu za  ripoti ya CAG sawa kuondoa sintofahamu iliyobainika. 

Kwa mujibuwa CAG wakati anawalisha ripoti hiyo alisema kuwa "Mheshimiwa Rais, nilibaini Chama cha Wananchi CUF kilipokea ruzuku toka Serikalini ya kiasi cha Shilingi milioni 369.38. Lakini Chama hicho kilihamisha kiasi cha shilingi milioni 300 kutoka akaunti ya Chama kwenda akaunti binafsi ya mwanachama na kiasi cha shilingi milioni 69 kilitolewa kama fedha taslimu. Hata hivyo nyaraka za matumizi ya fedha hizo hazikuwasilishwa kwangu kwa ajili ya ukaguzi.” 

Akifafanua kuhusu ripoti ya CAG, Profesa Lipumba amesema kauli hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imeleta mtafaruku na sintofahamu kubwa kuhusu usimamizi wa fedha za Chama cha CUF.Hivyo ni vema wakaweka  sawa kumbukumbu zao kwamba  tukio hilo lilitokea Januari mwaka 2017. 

Ameongeza  wakati huo Chama chao kilikuwa katika mgogoro wa uongozi na akaunti za Chama katika Benki ya NMB zilikuwa na tishio la kuzuwiwa. 

"Naomba nikumbushe kuwa Desemba 2 mwaka 2016, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza uchaguzi mdogo wa Udiwani katika kata 22 za Tanzania Bara. Nikumbushe kuwa baadaye Tume ilifanya masahihisho na kueleza kuwa ni kata 20 ndizo zitakazohusika na uchaguzi mdogo. Pia CUF iliamua kushiriki uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Dimani, Zanzibar.Hatimaye Chama kilisimamisha wagombea 14 kati ya kata 20 zilizotangazwa kurejea uchaguzi. Upande wa Zanzibar CUF iliweka Mgombea Ubunge jimbo la Dimani,"amesema. 

Amesisitiza kuwa wakati uchaguzi mdogo unatangazwa, Chama hicho klikuwa hakipewi ruzuku ya Serikali na kwamba sababu walitaka kushiriki uchaguzi na hawakuwa na fedha, Desemba 28 mwaka 2016 alimuandikia Msajili wa Vyama vya Siasa kuiomba Ofisi yake ikipatie. 

 “Chama chetu fedha zitokanazo na ruzuku ya kila mwezi ya Chama toka Serikalini ili kiweze kushiriki kikamilifu katika chaguzi ndogo zilizo tangazwa kurejewa hapa nchini na kutekeleza Mpango Mkakati wa  Ujenzi wa Chama chetu.” 

Profesa Lipumba amesema Msajili wa Vyama vya Siasa aliridhia Chama chao kipate sehemu ya ruzuku ili kishiriki katika uchaguzi na kutekeleza shughuli za Chama. Fedha hizo ziliwekwa kwenye akaunti ya Chama ya Benki ya NMB, tawi la Temeke. 

 Amesema katika kipindi hicho  kulikuwa na tishio la aliyekuwa Katibu Mkuu kuzuia akaunti zetu zote za Chama upande wa Tanzania Bara zisifanye kazi. Katika hali hiyo Kamati ya Utendaji iliamua shilingi milioni 300 tulizoomba kwa ajili ya kugharamia uchaguzi zihamishwe kwenda kwenye akaunti ya mwanachama muaminifu ili zisije kukwama kwenye akunti ya Benki. 

"Mwanachama huyo ni Masoud Mhina Omari, aliyekuwa Naibu Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na sasa na Naibu Mkurugenzi wa Mafunzo, Itifaki na Udhibiti.Shilingi milioni 69 zilitolewa kama fedha taslimu kuanza kugharamia shughuli za kampeni za uchaguzi zikiwemo ziara za viongozi kwenda kwenye kata zenye uchaguzi mdogo,"ameongeza. 

Amesema kuwa fedha zote zilizowekwa kwenye akaunti ya Masoud Mhina Omari zilitumiwa na Chama katika masuala ya Uchaguzi na uendeshaji wa shughuli za Chama. Wakaguzi wa CAG waliokuja kutukagua walipewa maelezo haya na nyaraka za matumizi ya Chama ya mwaka 2016/17. 

"Chama kinamshukuru Masoud Mhina Omari kwa uaminifu wake. Hatua ya kuweka fedha kwenye akaunti yake ilitusaidia kukamilisha shughuli za Chama kwani baadaye Benki ya NMB ilizuwia kutoa fedha kwenye akaunti zetu zote za Tanzania Bara.Naomba nisistize tukio hili la kuhamisha fedha kwenda akaunti ya Masoud Mhina Omari lilitokea Januari 2017 kwa sababu ya tishio la kuzuia kutoa fedha toka akaunti za Chama," amesema Prof.Lipumba. 

Pia amesema mgogoro wa Chama umemalizika na taratibu za fedha zinazingatia kanuni za fedha za Chama na kwamba wamekubaliana na ushauri wa CAG kuwa “mifumo ya udhibiti wa fedha ndani ya chama iimarishwe kwa kufuata sheria na katiba ya chama." Hivi sasa Mhasibu anaandaa mfumo imara wa udhibiti wa fedha ndani ya Chama."
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad