Mshauri mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amemkaribisha katika chama hicho aliyekuwa mwanachama wa CCM, Bernard Membe lakini akimuonya asiwe na masharti.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi 4, 2020 katika mahojiano yanayofanyika katika ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Tabata Relini jijini Dar es Salaam.
Maalim amtoa kauli hiyo siku chache baada ya Membe katika mahojiano na Mwananchi kudai kuwa alifukuzwa CCM kutokana na nia yake ya kutaka kupambana na mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Membe na makatibu wakuu wawili wastaafu, Abdulrahman Kinana na Yusufu Makamba walifikishwa mbele ya kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu kujibu mashtaka ya kinidhamu.
Makada hao waliingia matatani baada ya sauti zao pamoja na za wanachama wengine watatu, kusambaa katika mitandao ya kijamii ikizungumzia kuporomoka kwa umaarufu wa chama hicho na uenyekiti wa Magufuli.