Maisha ni Mzuka na Matendo Yenye Nidhamu...Soma Visa Hivi vya Tajiri Beffet na Bondia Tyson Utajifunza Kitu
0
March 30, 2020
MWAKA 1952, Warren Buffett, alipomuoa mkewe wa kwanza, Susan Thompson, alimwambia “niamini, nitakuwa tajiri.” Wakati huo, Buffett alikuwa na umri wa miaka 21, mtoto wa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Marekani, Wilaya ya Pili, Nebraska, Howard Buffett.
Mwaka 2004, Susan alipofariki dunia, alimwacha Buffett, Warren wake, ni tajiri namba mbili duniani, nyuma ya Bill Gates. Hata sasa, Buffett ni tajiri namba nne duniani, akiwa na utajiri wa dola 88 bilioni, ambazo ni Sh203 trilioni.
Oktoba 2, 1980, kijana mwenye umri wa miaka 14, Mike Tyson, alikuwepo kwenye arena ya Caesars Palace, Las Vegas, Nevada, akimshuhudia master wake, Muhammad Ali, akipewa kichapo cha “Nyerere kwa Idi Amin” kutoka kwa bondia Larry Holmes.
Ali ni master wa Tyson. Ndiye alimfanya apende boxing. Holmes alipompiga Ali, Tyson alimwaga machozi. Kupigwa kwa Ali ni kupigwa kwake. Tyson alimwambia Ali, “nikiwa mkubwa nitampiga Holmes kukulipia kisasi.” Ali alitabasamu. Alimuona Tyson mtoto na alizungumza kitoto.
Januari 22, 1988, yaani miaka saba na miezi mitatu tangu ahadi ya Tyson kwa Ali, Tyson alikutana ulingoni na Holmes. Kabla ya pambano, Ali alimnong'oneza Tyson: “Uliniahidi utanipigia huyu mwanaharamu.” Tyson na kile kithembe chake, akamjibu: “Limeisha hilo!” Tyson mwenye hasira na uchu wa kulipa kisasi na deni, alianza mchezo.
Raundi ya nne, Tyson alimlambisha Holmes sakafu mara tatu. Pambano likaisha kwa KO. Tyson alilipa kisasi cha master wake. Alilipa deni la ahadi kwa Ali kwamba angempiga Holmes akikua.
Ni mzuka! Mara nyingi tunahitaji mambo mawili tu kwenye haya maisha. 1, Mzuka wa kufanikisha jambo. 2, Nidhamu ya huo mzuka.
Kile kinachokusukuma ujipige kifua na kusema “lazima niwe fulani”. Huo ndio mzuka wako. Sasa hakuna kingine utahitaji zaidi ya nidhamu ya huo mzuka. Nidhamu ni uaminifu kwenye mzuka wako.
Buffett alikuwa na mzuka wa utajiri, matendo yake yakaakisi nidhamu ya hali ya juu kutimiza mzuka wake. Vivyo hivyo Tyson, alijifua kwa nidhamu mpaka akampiga Holmes. Na alimpiga kila aliyepanda naye ulingoni. Akaitwa "The Baddest Man On The Planet". Ni Mzuka Jumlisha Matendo Yenye Nidhamu.
Ndimi Luqman MALOTO
Tags