Man City imechukua Ubingwa, Bao la Kuchumpa la Samatta Laiteka Wembley


LONDON, ENGLAND. INAWEZEKANA Aston Villa imekosa ubingwa wa Kombe la Ligi, lakini Watanzania wengi wanasema potelea mbali maadam nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta amefunga bao katika pambano hilo kwao ni raha tu.

Katika mechi ya jana iliyopigwa katika Uwanja wa Wembley, Aston Villa ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Man City na kupoteza nafasi ya kutwaa taji la michuano hiyo, huku Samatta akiandika historia ya kwa Mtanzania wa kwanza kufunga bao katika Uwanja huo.
Japokuwa Watanzania wengi wamekuwa na mapenzi na Aston Villa tangu Samatta atue katika timu hiyo akitokea Genk wakati wa usajili wa Januari, kichapo cha jana hakikuwaumiza sana kwa sababu bao la Mbwana kwao lilikuwa kama ushindi.

Man City ndiyo ilikuwa wa kwanza kupata bao katika mchezo huo kupitia kwa Sergio Aguero aliyemalizia pasi ya kichwa ya kinda Phil Foden dakika ya 20 ya pambano hilo lilishuhudia Samatta akiandika rekodi kibao.

Dakika 10 baadaye, Man City waliongeza bao la pili kupitia kwa Rodri Hernandez aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi ya Ilkay Gundogan katika dakika ya 30 ya mchezo huo na kufanya matokeo kuwa magumu zaidi kwa Aston Villa.

Lakini, wakati wengi wakiamini Man City itashinda pambano hilo kiulaini Samatta aliwainua vitini mashabiki wa Aston Villa baada ya kupiga bao kali la kichwa cha kuchumpa akimalizia krosi safi ya Anwar El Ghazi, katika dakika ya 41 ya pambano hilo.

Bao hilo la Samatta ambaye jana aliandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika Uwanja wa Wembley lilifanya mchezo huo kwenda mapumziko matokeo yakiwa 2-1, Man City ikiongoza.

Katika kipindi cha pili timu hizo zilishambuliana kwa zamu, huku Man City wakitawala nusu ya kwanza ya kipindi hicho na Aston Villa wakitumia dakika za lala salama kuishambulia kwa nguvu Man City, bila mafanikio.

Licha ya timu zote mbili kufanya mabadiliko katika kipindi cha pili cha pambano hilo matokeo yaliendelea kuwa vile vile hadi mwamuzi anamaliza mchezo huo.
Kwa upande wa Aston Villa, kocha Dean Smith alifanya mabadiliko ya wachezaji wawili kwa mpigo katika dakika ya 70 ya mchezo huo akimtoa Ahmed El Mohamady na El Ghazi nafasi zao zikachukuliwa na Conor Hourihane na Trezeguet. Huku akimtoa Samatta katika dakika ya 80 na nafasi yake kuchukuliwa na Keinan Davis.

Man City wao waliwatoa Gundogan, David Silva na Aguero na nafasi zao kuchukuliwa na Kevin De Bruyne, Bernardo Silva na Gabriel Jesus.
Kwa ushindi wa jana wa mabao 2-1, Man City imefanikiwa kutetea taji lake la Kombe la Ligi baada ya kutwaa taji hilo msimu uliopita.

Vikosi

Manchester City (Mfumo 4-3-3): Claudio Bravo; Kyle Walker, John Stones, Fernandinho, Oleksandr Zinchenko; Ilkay Gundogan/De Bruyne (58), Rodrigo, David Silva/Bernardo (77); Raheem Sterling, Sergio Aguero/Jesus (84), Phil Foden.

HIZI HABARI KAMA HIZI ZINAPATIKANA KWENYE APP YA UDAKU SPECIAL DOWNLOAD APP YA UDAKU SPECIAL BLOG <DOWNLOAD HAPA>

Aston Villa (Mfumo 4-2-3-1): Orjan Nyland; Matt Targett, Tyrone Mings, Bjorn Engels, Frederic Guilbert; Douglas Luiz, Marvelous Nakamba; Anwar El Ghazi/ Trezeguet (70), Jack Grealish, Ahmed Elmohamady/ Hourihane (70); Mbwana Samatta/Davis (80).
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad