DAYOSISI ya Italia iliyo karibu na Milan, imeripoti vifo vya mapadri 30 wakati huu wa mlipuko wa virusi vya corona.
Gazeti linalomilikiwa na mkutano wa maaskofu wa Italia, Avvenire, limetaja vifo 28 vya mapadri hao vimetokana na maambukizi ya virusi vya corona.
Pia limebainisha kesi mbili za vifo vilivyoongezeka vya Padri Guido Mortari, ambaye alifariki dunia kwa nimonia kabla ya kuchukuliwa vipimo vya corona na Padri Giorgio Bosini, ambaye alifariki dunia akiwa katika hali mbaya.
Kati ya mapadri hao wote, watatu walikuwa na zaidi ya miaka 70, na zaidi ya nusu walikuwa na zaidi ya miaka 80.
Padri mdogo kabisa kufariki dunia kwa maambukizi ya virusi hivyo ni Andrea Avanzini wa Dayosisi ya Parma, ambaye alikuwa na umri wa miaka 54.
Kulingana na askofu wa eneo hilo, mapadri 11 waliokufa wametoka katika Dayosisi ya Bergamo, na mapadri wengine 15 wamelazwa hospitalini.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, alimwita Askofu wa Bergamo, Machi 18 ili aelezee kwa ukaribu kuhusu wale wanaoteseka katika dayosisi hiyo.
“Papa Francis ameahidi kwamba atatubeba katika moyo wake na katika sala zake za kila siku.
“Baba Mtakatifu alikuwa ameguswa sana, alionyesha ukaribu na mimi, kwa mapadre, wagonjwa, wale wanaowajali na jamii nzima. Alitaka kupata maelezo kuhusu hali ambayo Bergamo inakabiliwa nayo, ambayo alikuwa amefahamishwa hapo kabla.
“Kwa ujumla amenitaka kuwa karibu na wale wote wanaougua na wengine wote kwa njia tofauti, na hasa wale wanaofanya kazi ya kishujaa kwa wengine kama madaktari, manesi, wahudumu, mamlaka za afya na vyombo vya sheria,” alisema Askofu Francesco Beschi wa Bergamo kupitia ujumbe wa simu wa video kwa waumini wa dayosisi hiyo.
Bergamo ni nyumbani kwa Papa John XXIII.
Askofu Beschi aliwataka waamini wa Kanisa Katoliki wa eneo hilo kumwomba Baba Mtakatifu John XXIII kwa kuugua kwao na kwa msaada.
Padri Remo Rota, ambaye ni Muitaliano aliyehudumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa miaka 38, alifariki dunia Machi 17 huko Bergamo baada ya kuchukuliwa vipimo na kuonekana ameambukizwa virusi vya corona. Alikuwa na umri wa miaka 77.
Mapadri sita wamefariki dunia katika Dayosisi ya Parma kwa virusi hivyo hivyo vya corona.
Miongoni mwao ni Padri Franco Minardi, ambaye amehudumu katika parokia hiyo kwa miaka 70, na Padri Nicola Masi, ambaye ni Mseminari wa Saveriani wa Parma, ambaye alipata kuhudumu Amazon.
Dayosisi ya Piacenza-Bobbio imeripoti vifo vya mapadri watatu, wakiwamo pacha wa miaka 87, Padri Mario Boselli na Padri Giovanni Boselli, ambao walifariki dunia ndani ya siku moja.
Dayosisi nyingine za Italia zilizo na vifo vya virusi vya corona vilivyoripotiwa ni Cremona, Milan, Lodi, Brescia, Casale Monferrato na Tortona.
Kutokana na hali mbaya ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Italia, huduma ya mazishi ya faragha hutolewa kwa marehemu, kwani sherehe zote za kidini za umma, pamoja na shughuli za harusi na mazishi zimepigwa marufuku na Serikali.
Nchini Italia hali bado ni mbaya, vifo vingine 627 vilivyotokana na virusi vya corona vimeripotiwa jana – ndani ya siku moja na kufanya jumla ya waliofariki dunia kufikia 4,032.
Taarifa zinaonyesha kuwa karibu watu 3,000 wamefariki dunia kwa ugonjwa huo nchini Italia chini ya mwezi mmoja baada ya wengine zaidi ya 35,700 kubainika kuwa na virusi hivyo.
Kwa sasa Italia ndiyo inayoongoza kwa kuwa na vifo vingi vilivyotokana na virusi vya corona duniani ikiizidi kwa mbali China ambako ugonjwa huo ulianzia Desemba mwaka jana.
OPEN IN BROWSER