Berlin, Ujerumani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema leo kuwa haki ya kutafiti kinga ya virusi vya corona haiuzwi baada ya habari kuwa Rais Donald Trump alitaka Marekani inunue haki peke dawa inayoweza kuwa kinga iliyotengenezwa na kampuni ya Ujerumani.
Kauli hiyo, iliyotolewa katika mahojianona kampuni ya habari ya Funke, imekuja wakati wanasayansi wakikimbilia kutengeneza kinga ya virusi hivyo ambavyo vimeshaua takriban watu 6,000 kote duniani na kusababisha mamilioni ya watu wafungiwe na kuyumbisha soko la dunia.
"Watafiti wa Ujerumani wanachukua nafasi kubwa katika utengenezaji wa dawa na kinga na hatuwezi kuruhusu wengine kuomba haki peke za matokeo yake," Heiko Maas aliiambia Funke.
Likikariri watu walio karibu na serikali ya Ujerumani, gazeti la Die Welt liliripoti awali kuwa Trump aliahidi dau la "mabilioni ya dola" ili Marekani ipatiwe haki hizo za kutafiti kinga na kampuni ya CureVac inayojihusisha na teknolojia ya virusi, akitaka iwe na haki "kwa ajili ya Marekani pekee".
"Ujerumani haiuzwi," waziri wa uchumi, Peter Altmaier aliliambia shirika la utangazaji la ARD jana, akitoa maoni yake kuhusu ripoti hiyo.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Ndani, Horst Seehofer alitakiwa kuthibitisha jaribio la kwenda mahakamani la kampuni hiyo ya Ujerumani.
"Naweza kusema tu kwamba nimesikia mara kadhaa leo kutoka kwa maofisa wa serikali kwamba hilo ndio shauri, na tutalijadili katika kamati ya dharura kesho," alisema.
CureVac ilisema katika taarifa yake kuwa "inajiweka pembeni kuzungumzia ubashiri na inakanusha tuhuma zozote kuhusu dau la kuchukuliwa kwa kampuni hiyo au teknolojia yake".