Jeshi la Marekani limefanya mashambulio ya anga dhidi ya wapiganaji wa Taliban nchini Afghanistan, saa kadhaa tu baada ya rais Donald Trump kusema kuwa alikua na "mazungumzo mazuri " na viongozi wa kundi hilo.
Marekani ilisaini mkataba na Taliban Jumamosi uliolenga kuleta amani kwa Afghanistan baada ya miaka kadhaa ya vita.
Lakini msemaji wa vikosi vya Marekani amesema mashambulio ya anga ya Jumatano ni kujibu hatua ya wapiganaji wa Taliban kuvishambulia vikosi vya serikali ya Afghanistan katika jimbo la Helmand.
Bado taliban hawajatoa kauli yoyote kuhusu shambalio hilo.
Haijafahamika wazi ikiwa kulikua na majeruhi.
Shambulio la Jumatano lilikua ni la kwanza kufanywa na Marekani dhidi ya Taliban katika kipindi cha siku 11, wakati makubaliano ya kupunguzwa kwa ghasia yalipoanza baina ya pande mbili kuelekea mkataba wa Jumamosi .
Katika ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa Twitter, Colonel Sonny Leggett, msemaji wa vikosi vya Marekani nchini Afghanstan , alisema kuwa lilikua ni "shambulio la kujilinda" lililolenga kuvuruga shambulio dhidi ya vituo vya ukaguzi vya vikosi vya taifa la Afghanstan.
Msemaji huyo aliongeza kuwa Marekani bado "inaheshimu mkataba wa amani" lakini ina wajibu wa kulinda washirika wake wa Afghanstan. Amesema kuwa Waafghanstan na Marekani walikua wameheshimu upande wao wa makubaliano, lakini Taliban walionekana kutaka kutumia vibaya fursa hiyo.
Jumanne pekee, alisema, Taliban walifanya mashambulio 43 kwenye vituo vya ukaguzi vinavyodhibitiwa na vikosi vya Afghanstan katika jimbo la Helmand.
"Tunatoa wito kwa Taliban kuacha mashambulio yasiyohitajika na kuheshimu ahadi zao. kama tulivyoonesha, tutawalinda washirika wetu. itakapohitajika kufanya hivyo,''aliandika.
Hadi sasa Taliban imekataa kuthibitisha au kukanusha kuhusika na mashambulio yoyote.
Maafisa wa Marekani na Afghastan kwa pamoja walisema kuwa wanatarajia kuwa na mkataba wa muda ambao ''ungepunguza mapigano'' yaliyosababisha kufikiwa kwa makubaliano ya Doha na kuendelea baadae. Lakini makubaliano hayazungumzii lolote kuhusu usitishwaji wa mapigano iwapo Taliban wangeshambulia washirika wa Marekani jambo linaloleta mkanganyiko nchini humo.
Mashambulio ya sasa yanayofanywa na Taliban yanaweza kuangaliwa kama jaribio la makundi ya uasi la kuishinikiza serikali ya Afghanstan kuwaachilia huru maelfu ya wafungwa wa Taliban. Wanadai kwamba hilo liwe limetekelezwa kabla ya kuanza kwa "mazungumzo ya Wataliban wa tabaka mbali mbali " na serikali ya viongozi wengine wa kisiasa wa Afghanstan. Lakini hadi sasa rais Ashraf Ghani amekataa kuafiki kufanya hilo.
Hata hivyo , inawezekana pia kwamba mpango wa Taliban ni kuendelea na ''mapigano katika kipindi chote cha mazungumzo ya makundi mbali mbali ya Afghanstan'' ili kusisitizia misimamo yao ya mazungumzo na kuendelea kuwaunganisha na kuwahamasisha wapiganaji wao.