KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael amejiapiza kuwa atapambana kufa au kupona kuhakikisha wanamaliza msimu huu wa Ligi Kuu Bara katika nafasi ya pili inayoshikiliwa na Azam FC yenye pointi 54.
Hiyo ni baada ya kukata tamaa ya kuuchukua ubingwa wa ligi hiyo unaotarajiwa kwenda Simba inayoongoza ikiwa na pointi 71, huku Yanga wakiwa wa tatu wenye pointi 51, ikifuatiwa na Namungo FC yenye pointi 50. Mbelgiji huyo alijiunga na timu hiyo katikati ya msimu akichukua nafasi ya Mkongomani, Mwinyi Zahera aliyesitishiwa mkataba wake kwa kile kilichotajwa mwenendo mbaya wa timu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kocha huyo tayari amepata dawa ya kupata matokeo mazuri katika michezo inayofuata ya ligi na Kombe la FA ili kuhakikisha wanafi kia mafanikio yake aliyojiwekea msimu huu.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kikubwa alichokigundua ni wachezaji wake kucheza bila ya kufuata maelekezo, kitu ambacho ameanza kukifanyia kazi ili kuhakikisha wanafanikiwa kupata ushindi katika michezo yote inayofuata na lengo ni kuwaondoa Azam katika nafasi ya pili ili wakae wao.
“Kocha wetu ameweka malengo mawili katika msimu huu baada ya kuona timu haina nafasi ya kuchukua ubingwa, na kikubwa alichokipanga ni kuhakikisha anaifunga Simba huku akitaka timu imalize ligi ikiwa katika nafasi ya pili. “Kocha huyo tayari ameanza mikakati ya kuhakikisha anawaondoa Azam katika nafasi ya pili ili ikae Yanga, katika kufanikisha hilo kocha ameitisha kikao cha dharura leo (jana) kitakachowashirikisha wachezaji na benchi la ufundi.
“Katika kikao hicho mengi yatazungumzwa, lakini hilo ni la kwanza, lengo ni kuona kocha huyo timu yake inamaliza ligi ikiwa katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi, kocha ana imani kubwa na wachezaji aliokuwa nao watafanikisha hilo,” alisema mtoa taarifa hii.
Ofi sa Habari wa Yanga, Hassani Bumbuli alithibitisha hilo kwa kusema kuwa: “Ni kweli kipo kikao hicho cha kocha na wachezaji kitakachofanyika leo (jana) jioni, kipi kinazungumzwa bado sijafahamu, hivyo tusubirie taarifa itatolewa rasmi.”