Mshambuliaji hatari wa klabu ya Aston Villa na timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta anatarajiwa kuweka historia nyingine hii leo siku ya Jumapili ya tarehe 1/ 03/ 2020 kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza fainali ya Carabao Cup katika dimba la Wembley nchini Uingereza. Na ili kuandika ‘record’ kubwa zaidi kwa nyota huyo hakuna namna lazima City wapigwe tu.
Samatta ashuka uwanjani akiwa na waajiri wake hao wapya, Aston Villa kukabiliana na Manchester City, huku nyota huyo kutoka Afrika Mashariki akitarajiwa kuwa ndiye mshambuliaji tegemeo akiwa amefunga bao moja katika michezo mitatu aliyoichezea timu hiyo hya England.
Kuelekea mchezo huo, Samatta amesemakuwa anajisikia mwenye bahati kubwa kwani amecheza mechi mbili tu na amefanikiwa kuingia fainali, “Maandalizi ya mchezo huu ni makubwa na ninaona kabisa kuanzia kwenye mazoezi kuwa tunakabiliana na changamoto kubwa, nasi tumejiandaa kwenye mchezo huu“.
“Ni habari njema sana kwangu, nimejiunga na klabu na baada ya mechi mbili tu ninacheza fainali. Ni wakati mzuri sana kwangu“, ameongeza Samatta.
Mara ya mwisho kwa Aston Villa kushinda taji ni mwaka 1996, iliposhinda kombe la ligi kwa kuifunga Leeds United. Inakutana na Manchester City ambayo ni bingwa mtetezi wa kombe la Carabao huku kocha wa Man City, Pep Guardiola akiwa na rekodi nzuri kuelekea fainali hiyo kwani mpaka sasa amecheza jumla ya fainali 24, akishinda 20 na kupoteza fainali nne pekee.