Baada ya kufanikiwa kulipiwa faini zao siku ya jana, leo Wabunge wa CHADEMA Ester Bulaya, Ester Matiko na Halima Mdee, wametoka gerezani na kuzungumza na waandishi wa habari, hali iliyopelekea Mdee kumwaga machozi akieleza kushangazwa na upendo wa wananchi.
Wakizungumza leo Machi 12, 2020, kwa nyakati tofauti katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho Mtaa wa Ufipa jijini Dar es Salaam, ambapo Ester Bulaya amesema kuwa kwa sasa safari yake ya mapambano ndiyo imeanza.
"Suala la kwamba eti nilifungwa ili nirudishe nyuma mapambano, hiyo siyo 'slogan' ya Ester Bulaya,ninachoamini nilienda kupumzika na sasa nimetoka tuanzishe tena mapambano upya" amesema Ester Bulaya.
Akizungumza kwa uchungu Halima Mdee amesema, "Ile adhabu pale haikuwa bahati mbaya, wanajua hatuna hata 100, lakini Watanzania nyie hamjui mlivotustiri, mimi ni kamanda lakini napata hisia, najua watu walivyo na hali mbaya watakuwa wamekata tamaa, nalia siyo sababu ya hofu, kule gerezani wanaujua mziki wetu".
Aidha kwa upande wake Mbunge wa Tarime Mjini Ester Matiko, amewashukuru wananchi wote waliojitoa kwa ajili yao na kwamba waendelee kuchangia ili na viongozi wengine waweze kutoka.