Mike Tyson: Nakisubiri Kifo kwa Hamu


Bingwa wa zamani wa ndondi za uzito wa juu duniani Mike Tyson amesema anasubiri kwa hamu kifo chake kwa kuwa “kuishi kunaweza kuwa ni kugumu kuliko kufa”.

Tyson bado anashikilia rekodi ya kuwa bingwa wa uzito wa juu duniani mwenye umri mdogo zaidi alimpomtwanga Trevor Berbick kwa “knockout” mwaka 1986 akiwa na umri wa miaka 20 na miezi minne.

Tyson, mwenye umri wa miaka 53, alisema katika mahojiano na tovuti ya The Sportsman la Uingereza kwamba anaamini kutoogopa kwake jambo lolote kulimfanya awe tayari kwa kifo ulingoni ingawa aliamini ni yeye ndiye angeua kama kungetokea kifo katika moja ya mapambano yake.


“Nilijua kwamba kuna uwezekano wa mimi kufa wakati wa mazoezi au wakati wa pambano, lakini sikuwa na hofu yoyote kwa kuwa niliamini kwamba kama kuna mtu angekufa, ni mimi ndiye ningeua. Kujiamini huko kulikuwa ni mbinu ya kujinusuru.

“Lakini sasa, kutokana na uzoefu na kutokana na kile ninachoamini, kila ninapofahamu zaidi kuhusu kutokuwepo duniani ndipo ninapokuwa tayari zaidi kufa.”

Alipoulizwa endapo ni kweli anasubiri kifo chake kwa hamu, mbabe huyo wa “knockout” alisema: “Ndio, siogopi. Kuishi kunaweza kuwa ni kugumu kuliko kufa. Ndivyo ninavyoamini. Sijui kama ni kweli. Kwa sababu kuishi kunahitaji ujasiri. Bila ujasiri, huwezi kumudu kuishi.

“Maisha ni safari, maisha ni mapambano. Watu wana kila kitu, lakini bado maisha yanakuwa magumu kwao,” alisema Tyson.

Tyson hivi karibuni alimwaga chozi na kusema anaona maisha yake yamekuwa “matupu” akikumbuka wakati wake kama mmoja wa wanamichezo maarufu zaidi duniani, na kwamba anakumbuka kwa uchungu enzi za ubabe wake ulingoni ambapo alikuwa hapigiki.


Mmarekani huyu alikuwa bingwa wa dunia mara mbili, lakini alikaa jela miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia ya ubakaji mwaka 1992.

Baada ya kuachiwa huru, alitwaa mataji ya WBC na WBA mwaka 1996, lakini mwaka huohuo aliyapoteza kwa Evander Holyfield ambaye aling’atwa sikio na Tyson katika pambano la marudiano mwaka uliofuata.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad