MKAZI wa Mgongoro wilayani Igunga mkoani Tabora, Muya Kasanzu (48), anadaiwa kuuawa kikatili kwa kucharangwa mapanga, huku mtoto wake Abdallah Muya (17), akijeruhiwa usoni vibaya na watu watatu wasiojulikana.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mgongoro, Kalolo Masubi alisema tukio hilo liliokea saa 7 usiku, Machi 21, mwaka huu. Alisema watu watatu wakiwa na mapanga na fimbo, walivamia nyumbani kwa marehemu kisha kumshambulia kwa mapanga na fimbo hadi kufa.
Alisema wakati wakimshambulia, marehemu alipiga kelele mara moja ya kuomba msaada na wananchi walifika eneo la tukio na kukuta amefariki. Alisema pamoja na watu hao kumuua, kisha kumjeruhi usoni mtoto wao wenyewe walipiga simu polisi na walipofika walikuta watu hao wamekimbia.
Alisema chanzo cha mauaji hayo, ni migogoro ya mashamba ambayo imeshamiri eneo hilo. Alisema marehemu wakati wa uhai wake, alikuwa na kesi mjini Tabora na baadhi ya wakulima wenzake ambapo kesi hiyo ilikuwa isikilizwe Machi 27, mwaka huu.
Mtoto wa marehemu, Muya alisema yeye na mdogo wake, Hassani walikuwa wamelala ndani ya nyumba moja ambayo upande mmoja ukuta wake ulikuwa umeanguka kutokana na mvua inayoendelea kunyesha, walilazimika kuegesha miti.
Alisema saa 7 usiku, waliona watu watatu wakiwa na mapanga na fimbo wakiingia ndani, baada ya kuusukuma miti na ndipo wakaanza kumkata mapanga na kumpiga fimbo baba yao huku mdogo wake akifanikiwa kutoka baada ya kufanikiwa kumsukuma mmoja wapo ya watu hao.