Morrison: Mashabiki wa Yanga Walinipa Wazimu



KIUNGO fundi wa Yanga, Bernad Morrison amefunguka uwepo wa mashabiki wengi wa Yanga, katika mchezo wao dhidi ya Simba, ulimpa morali kubwa kiasi cha kuhisi anaweza kufanya kila kitu uwanjani.

 

Morrison amesema ushindi waliopata mbele ya Simba ulichagizwa pakubwa na shangwe na kelele zilizopigwa na mashabiki wa Yanga katika dakika zote 90, huku akifunguka kuwa hakutarajia kama mashabiki hao wangekuwa ‘vichaa’ wa soka.

 

Morrison ndiye aliyeipa ushindi Yanga wa bao 1-0, mbele ya Simba katika mchezo uliochezwa Machi 8, katika Uwanja wa Taifa na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Ahmad Ahmad.



Akizungumza na gazeti hili, Morrison alisema: “Mashabiki wa Yanga walikuwa katika ubora wao, walipiga kelele ambazo mimi binafsi ziliniongezea morali na kuona kuwa naweza nikafanya kila kitu nikiwa na mpira.

 

“Kiukweli niwashukuru sana, maana kila mchezaji wa Yanga alionekana kuwa na nguvu sana, ushindi tuliopata ulisababishwa na nguvu yao.



“Niwaombe wasiache kufanya hivyo, ilinishangaza sana, ukishika mpira wanashangilia, ukiwa unashambulia wanashangilia, ilinipa maswali sana kuwa walikuwa wanahitaji nini, nikagundua kuwa wanahitaji bao na kwa bahati nzuri nilifanya hivyo, lakini kiukweli walinipa hamasa kubwa sana, ninawashukuru sana,” alisema Morrison.

Stori: Issa Liponda, Dar es Salaam


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad