SIKU moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumvua uanachama aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Katibu wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wastaafu wa chama hicho, Pius Msekwa, amesema kitendo hicho ni utekelezaji wa wajibu wa kawaida na wa kila siku wa chama hicho.
Juzi Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu iliyoketi chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. John Magufuli, imefikia uamuzi wa kumvua Membe uanachama kwa makosa ya kimaadili.
Alisema Membe ameonekana kushindwa kujirekebisha kutokana na adhabu alizowahi kupewa kipindi cha nyuma.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Msekwa ambaye pia ni Spika wa Bunge mstaafu, alisema utaratibu wa kuwavua uanachama wanaokwenda kinyume na maadili ya chama hicho, umekuwapo tangu wakati wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na kwamba viongozi mbalimbali wamewahi kuvuliwa uanachama.
“Utaratibu huu umeanza tangu wakati wa Tanu, Maalim Seif akiwa CCM alifukuzwa uanachama, Oscar Kambona alikuwa Katibu Mkuu wakati ule wa Tanu alivuliwa uanachama, kwa hiyo ni utaratibu wa kawaida wa chama na wa kila siku,” alisema Msekwa.
Kuhusu athari ambazo chama hicho kinaweza kupata kwa kumvua uanachama mwanachama aina ya Membe, alisema hakuna athari yoyote huku akihoji kuwa wale waliovuliwa uanachama hapo kabla walisababisha athari gani.
“Hao niliokutajia walileta athari gani kwa chama? Wewe uliona athari yoyote? Huu ni uamuzi sawa na wa mahakama, mtu anaitwa kwa kanuni anahojiwa, kama amekiuka kanuni za chama anavuliwa uanachama,” alisema Msekwa.
Alipoulizwa kuhusu ugumu wa kutoa uamuzi wa kumvua uanachama mwanachama wa aina ya Membe, alisema kuwa hakuna ugumu wowote kwa sababu kinachoangaliwa ni kama mwanachama husika amekiuka katiba ya chama.
Licha ya chama hicho kumvua Membe uanachama, pia kilimpa karipio na kifungo cha miezi 18 Katibu Mkuu mstaafu, Abdulrahaman Kinana, ambaye kwa muda huo hataruhusiwa kuwania nafasi yoyote ndani ya chama hicho, huku kikimsamehe Katibu Mkuu mstaafu, Yusuf Makamba, baada ya kuomba msamaha kwa barua.
Makada hao wote walifikishwa katika Kamati ya Maadili ya chama inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Dk. Philip Mangula kuhojiwa kwa makosa ya ukiukwaji wa kimaadili.
Maazimio ya kuwaita yalifikiwa Desemba 13 mwaka jana na Halmasharui Kuu ya CCM iliyokutana jijini Mwanza chini ya Mwenyekiti wake Rais Magufuli.
Sababu ya kuitwa kwa makada hao ni baada ya Julai mwaka jana sauti zao kusambaa katika mitandao ya kijamii zikimsema vibaya Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM.
Wengine waliohusishwa na sauti hizo ni Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngereja ambao kwa nyakati tofauti waliomba radhi na kusamehewa.
Baadaye ulisambaa waraka wa Kinana na Makamba wakieleza kuwa katika hatua yao ya kuuandika walizingatia Katiba ya CCM toleo la mwaka 2017 ibara ya 122.
Katika waraka huo, wazee hao waliliomba baraza hilo kushughulikia shutuma ambazo zilielekezwa kwao na mtu aliyejitambulisha kama mtetezi wa Serikali, akiwatuhumu kwa mambo waliyodai ya uzushi na uongo jambo ambalo lilielekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani na nje ya chama.
Akizungumzia suala hilo wakati huo, Msekwa alisema wanasubiri vikao vya chama kuamua juu ya kile kilichoandikwa katika barua ya malalamiko ya makatibu wakuu hao wastaafu, kwamba wamedhalilishwa kwa mambo ya uzushi na uongo.
Msekwa alisema barua hiyo ambayo ni ya kwanza kuwafikia wao kama Baraza la Wazee Wastaafu na kwamba kwa kawaida itapelekwa kwenye chama hicho ambacho ndicho kinachopaswa kuitisha vikao kushughulikia malalamiko yaliyotajwa, huku akidai kuwa ilikuwa mara ya kwanza kupokea malalamiko ya aina hiyo.
Alipoulizwa ni kwanini walishindwa kukemea suala hilo kabla ya kupelekewa barua hiyo, alisema kwa mujibu wa Katiba ya CCM kazi yao ni kutoa ushauri na kwamba ushauri hautolewi kama amri bali unaombwa.