Zororo MAKAMBA, mtangazaji kijana umri wake miaka 30 amefariki dunia kwa ugonjwa wa Corona nchini Zimbabwe. Taarifa za kifo chake zimestua wengi nchini humo kikiwa ni kifo cha kwanza kilichotokana na Virusi vya Corona katika taifa hilo la Kusini mwa Afrika.
Zororo mtangazaji wa redio na runinga, alikuwa akitazamwa na wengi kama kipaji halisi kilichobeba nguvu na maono makubwa ya kihabari. Ni mtoto wa mfanyabiashara maarufu na Mbunge wa zamani wa ZANU-PF, James Makamba. Zororo alilazwa juzi Jumamosi katika Hospitali ya Wilkins mjini Harare, Zimbabwe hali yake ikielezwa kubadilika ghafla.
Amepata kuendesha vipindi mbalimbali maarufu kama State of the Nation, Point of View na kuongoza vipindi vya matukio katika ZiFM Radio. Hadi anafariki alikuwa na mkabata na serikali wa kufafanua masuala mbalimbali ya kitaifa kupitia video. Zororo Makamba alizaliwa Januari 17, 1990 na alikuwa msomi wa Shahada ya Kwanza ya Mawasiliano kwa Umma kutoka Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani.