Na James Timber, Mwanza
Mkuu wa majeshi nchini Jenerali Venance Mabeyo amefanya ziara mkoani Mara kwenye eneo linalotarajia kujengwa kituo cha kikosi cha jeshi la majini kutokana na eneo linalotumiwa sasa kuingiliwa kwa shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi wa taasisi jirani na kulifanya kuwa finyu.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa eneo hilo, amewataka wananchi watarajie kupokea kikosi hicho katika eneo la Nyabange wilayani Butiama na kuhimiza kutoa ushirikiano ili kudumisha suala la ulinzi wa mipaka kitaifa na usalama wa wavuvi ziwa viktoria.
"Hili eneo linatufaa katika shughuli zetu tunatarajia watanzania wazalendo watatoa ushiriakiano wa kutunza mipaka lisiingiliwe kama lile la bandari pia viongozi wa serikali ngazi za vijiji naombeni muwape wakazi jirani elimu juu ya eneo hili wakae mbali kama sheria inavyoelekeza," amesema Mabeyo.
Pia ameeleza kuwa Mkoa wa Mara unapakana na nchi mbili ambazo ni Uganda na Kenya kuwepo kwa eneo hilo kutasaidia kujiimarisha kiulinzi kwani vifaa vitavyotumika hapo vitakuwa bora zaidi tofauti na sasa.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima amempongeza mkuu huyo wa majeshi kuafiki kuwepo kwa jeshi la wanamaji katika eneo hilo kwani itakuwa chachu ya kuinuka kiuchumi kupitia raslimali za ziwa victoria ambapo wavuvi wataepukana na uvuvi haramu na kuvua uvuvi unaoendana na sheria taratibu na kanuni za nchi kwani askari hao watasimamia na kupinga uvuvi haramu.
Naye Wambura Samweli Mkazi wa Nyabange ambaye amesema alipata eneo hilo mwaka 1986 lenye ukubwa wa hekta 95.3 na kugawa hekta 55 kwa jeshi la wananchi ili kuboresha ulinzi huku akisubiria taratibu za kiserikali kwa ajili ya malipo ya fidia.