Nabii Joshua Kufanya Maombi Akiwa Amevalia Magunia Siku 40 Hadi Corona Iondoke Katika Uso Wa Dunia



Na Mwandishi Wetu, Morogoro
KIONGOZI Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala ametangaza siku 40 za kuvaa magunia akiwa katika maombi hadi hapo virusi vya corona (COVID-19) vitakapoondoka katika uso wa Dunia.

Nabii Joshua alitangaza hatua hiyo jana mjini Morogoro wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea juu ya maono na wito huo ambao Mungu amempatia ili kufanya maombi mfululizo hadi ugonjwa huo utakapoondoka.

Alisema, amefikia hatua hiyo baada ya Roho Mtakatifu kumuonyesha kwamba Taifa la Tanzania na Dunia imefika mahali ambapo inahitaji msaada wa Mungu.

Pia alitoa wito kwa Watanzania wakati wakiendelea kumuomba Mungu kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia maelekezo ya Serikali juu ya COVID-19 na kuchukua tahadhari kila wakati kwa kuwa, ugonjwa huo unaenda kutoweka katika uso wa Dunia.

"Nichukue nafasi hii pia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kweli anahitaji pongezi kabisa. Na ameishangaza Dunia kwamba Tanzania hatutapiga saluti mbele ya shetani Corona tukaacha kumuabudu Mungu,"alisema Nabii Joshua.

Alisema, kuanzia leo kila Mtanzania kwa imani yake ashiriki kumuomba Mungu ili aweze kuiondolea Tanzania na Dunia majanga mbalimbali ikiwemo Corona ambao umewapa hofu watu, jambo ambalo kwa Mungu haliwezi kushindwa kupata ufumbuzi.

"Rais Magufuli ni rais pekee duniani aliyesema tutamuabudu Mungu wetu na tutamuomba Mungu aweze kukomesha tatizo kubwa la Corona, hili ni jambo kubwa, nataka kutafsri lugha yake kwa umma, natafsri lugha yake kwa umma kwa sababu watu wengi wamelichukulia jambo hili kuwa ni jambo la kawaida sana, kwa mujibu wa Biblia maandiko yanasema, mioyo ya wafalme ipo mikononi mwa Mungu.

"Naye huiongoza atakako kama maji, ukisoma Warumi 13 anasema mamlaka zote zinatoka kwa Mungu kwa hiyo na hii iliyopo sasa inatoka kwa Mungu.

"Kwa hiyo kiongozi yeyote mkubwa wa Taifa huwa anakuwa na roho maalum kutoka kwa Mungu ndani yake kwa ajili ya kuongoza ile jamii na kuwapa ile jamii wanachostahili kupewa.

"Kwa hiyo tunaamini kabisa kwamba kauli ya Rais Magufuli kuhusu ibada ni rufaa juu ya sayansi kwani sayansi inaposhindwa rufaa yake ni imani, Biblia na historia inaonyesha hivyo, zamani kulikuwa na magonjwa makubwa sana ambayo yaliitwa tauni katika Biblia, yaliua maelfu ya watu, sayansi zilikoma, watu wataalamu wa dunia walishindwa.

"Ndipo Mfalme Daudi akavaa gunia kama nilivyovaa leo, alipovaa gunia akamlilia Bwana, ndipo Bwana akampa uwezo wa kujenga madhabau kwenye uwanja wa Harauna, hatimaye Mungu akarudisha hasira zake na nchi ikapata uponyaji. Hivyo ndivyo inavyokwenda kuwa katika uso wa Dunia, corona itaondoka na nchi zitapata uponyaji,"alifafanua Nabii Joshua.

Alisema, licha ya mataifa makubwa ikiwemo Marekani, China na Italia kuonekana kushindwa katika kudhibiti Corona, anaamini ndani ya siku 40 za kuvaa gunia huku akifanya maombi adui huyo ataondoka kwa jina la Yesu.

"Ninao wito mkubwa sana kwa ajili ya Taifa la Tanzania na nimepewa dhamana kubwa sana kwa ajili ya kulitegemeza Taifa la Tanzania. Nitaendelea kufanya maombi mfululizo kwa ajili ya uponyaji wa Taifa letu, Dunia na kila mmoja na hakika Mungu atazidi kumuonekania kila mmoja wetu,"aliongeza Nabii Joshua.

Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania inayoongozwa na Nabii Joshua ambayo ina makao yake makuu Yespa, Kihonda mjini Morogoro pia inaratibu kampeni ya Kitaifa ya kuliombea Taifa ambayo imekuwa na mafanikio makubwa tangu izinduliwe na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai jijini Dodoma hivi karibuni.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad