Dar es Salaam. Ibrahim Mbita amesema mdogo wake, Iddy amefariki kwa ugonjwa wa corona leo Jumanne Machi 31, 2020 katika kituo cha matibabu ya wanaougua ugonjwa huo kilichopo Hospitali ya Mloganzila, Dar es Salaam.
Ameeleza hayo leo wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu taarifa za msiba huo. Iddy ni Mtanzania wa kwanza kufariki dunia kwa ugonjwa huo nchini.
Leo taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu imethibitisha kifo hicho na kubainisha kuwa alikuwa akipatiwa matibabu katika kituo hicho.
"Marehemu ni Mtanzania mwanaume mwenye umri wa miaka 49 ambaye pia alikuwa akisumbuliwa na maradhi mengine."
"Tunamuomba Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi, na tunatoa pole kwa familia, ndugu jamaa wa marehemu, " amesema Ummy.
Amesema hadi leo asubuhi watu 19 wameambukizwa corona, aliyepona ni mmoja na kifo ni kimoja.
Jana, Ummy alieleza kuwa kuongezeka kwa wagonjwa watano wa corona wakiwamo wawili waliokuwa wakifuatiliwa na kufanya idadi ya waliobainika kuwa na maambukizi nchini kufikia 19.
Amesema mgonjwa wa pili ni mwana mke mwenye miaka 21 Mtanzania ambaye ni miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatiliwa.
Kuhusu mgonjwa wa tatu, Ummy amesema ni mwanaume mwenye umri wa miaka 49 Mtanzania ambaye pia ni miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatiliwa.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi