Polepole afunguka sababu ya JPM kumlipia faini Mchungaji Msigwa
0
March 13, 2020
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole amesema uamuzi wa mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli kumlipia faini ya Sh38 milioni mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ili atoke gerezani haupaswi kuchukuliwa kisiasa.
Amesema aliyemlipia faini mchungaji Msigwa ni Rais Magufuli kwa sababu binti wa kiongozi mkuu huyo wa nchi ameolewa katika familia ya mbunge huyo.
Jana Alhamisi Machi 12, 2020 Rais Magufuli kupitia wasaidizi wake walieleza kulipa kiasi hicho cha fedha, ndugu wa Mchungaji Msigwa kuchangishana Sh2 milioni na kukamilika Sh40 milioni alizotakiwa kulipa mbunge huyo.
Hata hivyo, Chadema walisema walikuwa wameshalipa faini ya Mchungaji Msigwa na kubainisha kuwa hawakuwa wakifahamu chochote kwamba amelipiwa, kama angekuwa amelipiwa mahakama ingewarejeshea fedha zao.
Mchungaji Msigwa ni kati ya viongozi nane wa Chadema ambao pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji Jumanne Machi 10, 2020 walihukumiwa kulipa faini ya Sh350 milioni au kwenda jela miezi mitano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliyokuwa yanawakabili.
Washtakiwa hao wakiongozwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walilazimika kwenda jela baada ya kushindwa kukamilisha taratibu za kulipa faini hiyo waliyohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Tags