RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta juzi aligeuka kuwa mchuuzi wa maandazi baada ya kukabidhiwa ndoo ya maandazi na mama mmoja katika barabara ya Nairobi – Nanyuki.
Kenyatta ambaye alikuwa akielekea Nyeri kukagua miradi ya maendeleo ya serikali, alikutana na wafuasi wake katika barabara hiyo na aliposimama kuwasalimia, ndipo mama huyo alipomkabidhi ndoo hiyo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, Uhuru alibeba ndoo hiyo na kuanza kuwagawia wafuasi wake maandazi hayo aliyoyanunua kwa mchuuzi huyo.
Uhuru aliwasili mjini Nanyuki, kaunti ya Laikipia na kutangaza kwamba alikuwa safarini kuelekea Nyeri kukagua miradi ya serikali.
Akiwa Nanyuki, kiongozi huyo wa taifa alikaribishwa na mamia ya vijana ambao alitangamana nao na kupiga nao soga.
Kwenye video iliyosambaa mitandaoni, Uhuru alionekana akiwagawia wafuasi wake andazi moja moja kabla ya kuwaaga na kuondoka.
Safari hii rais hakuwa ameandamana na walinzi wake wote kama ilivyo ada wakati anapozuru maeneo mbalimbali nchini au katika hafla za kitaifa.
“Nataka kila mtu awe na uhuru wa kuishi katika sehemu yoyote ya nchi. Hizi taarifa zote, propaganda zote mnazozisikia kuhusu BBI, ni za kupotosha tu,” alisema.