Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameagiza kupulizwa dawa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kuanzia kesho, ili kuua vijidudu vinavyoeneza magonjwa vikiwemo virusi vya corona ambavyo vimeathiri watu kumi na wawili nchini hadi sasa.
Makonda ameyasema hayo alipotembelea kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo, lengo likiwa ni kujiridhisha kama watoa huduma katika kituo hicho wanachukua hatua za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Amewaeleza wasafiri waliokuwepo kituoni hapo kuwa virusi vya corona ni hatari, hivyo wachukue tahadhari kwa kujikinga wao wenyewe pamoja na kuwakinga wengine.
Aidha, amewataka wakazi wa mkoa huo wa Dar es salaam kutoa taarifa mapema endapo watabaini kuwepo kwa mtu mwenye dalili zinazofanana na za mgonjwa wa homa ya corona, na kwa mtu anayehisi kuwa na dalili za homa hiyo atoe taarifa ili aweze kupatiwa huduma zinazostahili.