Ripori Ya CAG Yabaini Ubadhirifu CUF, CCM



Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amebainisha ubadhirifu kwenye vyama vya siasa wakati akikabidhi ripoti za ukaguzi wa hesabu za Serikali na taasisi za umma kwa mwaka 2018/2019.

Akiwasilisha ripoti hiyo kwa Rais John Magufuli leo Alhamisi Machi 26, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, CAG amesema katika ukaguzi ilibainika kuwa Chama cha Wananchi (CUF) kilipokea ruzuku ya Sh milioni 369.38 lakini Sh milioni 300 zilihamishwa kwenye akaunti ya chama na kuwekwa katika akaunti binafsi na Sh milioni 69 zilitolewa kama fedha taslimu.

Kichere amesema nyaraka za matumizi ya fedha hizo hazikuwasilishwa kwake kwa ajili ya ukaguzi.

“Nilibaini Sh milioni 47 zilitolewa kwenye akaunti ya chama bila idhini ya Katibu Mkuu wa chama kama ilivyoelekezwa katika kanuni za fedha za chama cha wananchi.

“Ninashauri mifumo ya udhibiti wa ndani ya chama cha CUF uboreshwe ili kuhakikisha matumizi yanazingatia kanuni zilizowekwa,” amesema CAG.

Aidha amesema alibaini Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ilimwondoa mpangaji bila kufuata taratibu na kusababisha mpangaji huyo kuonesha nia ya kufungua kesi ya madai na kutaka kulipwa fidia ya Sh milioni 800, hata hivyo jumuiya hiyo ililipa kiasi cha Sh milioni 60 kama fidia ya hasara baada ya mazungumzo ya kirafiki kufanyika na suala hilo kumalizika nje ya mahakama.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad