TANZIA: Nyota wa muziki wa country Kenny Rogers afariki dunia
0
March 21, 2020
Nyota wa muziki wa country, Kenny Rogers, ambaye amekuwa katika muziki kwa miaka 60, amefariki akiwa na umri wa miaka 81, familia yake ilisema jana jioni.
"Rogers amefariki kwa amani akiwa nyumbani kwake na kifo chake ni cha kawaida. Amefariki akiwa chini ya uangalizi na akiwa amezungukwa na familia yake," imesema taarifa ya familia.
Mwimbaji huyo mzaliwa Texas alijulikana kwa nyimbo zake zilizotamba duniani kama "The Gambler," "Lucille" na "Islands in the Stream."
Familia ilisema ilikuwa inapanga kuwa na mazishi ya kifamilia kutokana na taifa la Marekani kuwa katika hali ya dharura baada ya mlipuko wa virusi vya corona.
Rogers, ambaye amewahi kutwaa tuzo za Grammy mara tatu, alilazimika kufuta ziara za mwisho za kuaga mashabiki kutokana na tatizo la afya mwaka 2018.
Rogers alianza muziki mwishoni mwa miaka ya hamsini na hakuchukua muda akaanza kuwa maarufu katika muziki wa rock, jazz na aina nyingine ambazo aliziingiza katika nyimbo zake za country.
Aliendelea kutamba na vibao vyake 24 vilishika nafasi ya kwanza katika chati za muziki, akishinda mara sita katika Tuzo za Muziki wa Country na kuingizwa katika Country Music Hall of Fame.
Mashairi yake mepesi ya mapenzi na kufanya ziara mara kwa mara vilimfanya apendwe na wengi.
Rogers pia alizidisha umaarufu wake aliposhirikiana na mwanamuziki nyota wa kike, Dolly Parton na kuonekana katika vipindi vya televisheni, kikiwemo cha "The Muppet Show."
Tags