TCRA yatangaza kushindanisha tuzo 17 sekta ya mawasiliano



Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TCRA imeanzisha mchakato wa kutoa tuzo za Teknolojia na Mawasiliano (TEHAMA) kwa wadau wake wenye leseni za TCRA.

Tuzo hizo zilizoandaliwa kwa jina la ‘TCRA ICT Awards 2020’ zina lengo la kuwatambua na kuwatunuku watoaji huduma bora zaidi za mawasiliano, kuongeza ubunifu, ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma za utangazaji na mawasiliano katika sekta mbalimbali lakini pia kutia chachu sekta ya mawasiliano na kukuza uchumi wa kidijitali.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa TCRA, Mhandisi James Kilaba wakati akizungumza na wahariri pamoja na waandishi waandamizi mapema leo Machi 5, 2020, ambapo amesema utoaji wa tuzo hizo itakuwa ni zoezi endelevu lenye lengo la kuhakikisha watoa huduma za mawasiliano wanatoa huduma katika viwango vilivyo bora zaidi.

Amesema, TCRA ICT Awards 2020 imeweka makundi 17 yatakayoshindanishwa katika tuzo hizo ambayo ni mtoa maudhui bora wa blog wa mwaka, mtoa huduma wa mtandao wa simu wa mwaka, mtoa huduma bora wa intaneti wa mwaka, mtoa huduma bora wa miundombinu ya utangazaji wa mwaka, kituo bora cha utangazaji wa televisheni cha kitaifa cha mwaka, kituo bora cha utangazaji wa televisheni cha wilaya cha mwaka, mtoa huduma bora wa kitaifa wenye maudhui yanayotazamwa kwa kulipa kwa njia ya satelaiti, chaneli bora ya kitaifa inayotazamwa kwa kulipia,

Makundi mengine ni kituo bora cha utangazaji wa redio cha kitaifa cha mwaka, kituo bora cha utangazaji wa redio cha kimkoa cha mwaka, kituo bora cha utangazaji wa redio cha kiwilaya cha mwaka,  kituo bora cha utangazaji wa redio cha kijamii cha mwaka, mtoa maudhui mtandao bora wa redio, wa mwaka.

Pamoja na huduma bora wa usafirishaji vifurushi na vipeto wa kimataifa wa mwaka, mtoa huduma bora wa usafirishaji vifurushi wa kimataifa wa mwaka, na mtoa huduma bora wa usafirishaji vifurushi na vipeto wa mji.

Kilaba amesema, mchakato huo ulianza tangu Januari 31, 2020 ambapo mshiriki anatakiwa kujaza fomu na mwisho wa uwasilishaji wa fomu hizo ili kuthibitisha ushiriki Machi 15, 2020.

Ameeleza kuwa mchakato wa kutafuta watoa huduma bora utahusisha wananchi ambao ni walaji wa huduma zinazotolewa ambapo watapiga kura kwa mtoa huduma bora.

Washindi wanatarajiwa kutangazwa Mei 15, 2020 ambapo zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi hao.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad