Tshishimbi Aikomoa Simba



KIUNGO mkabaji wa Yanga, Mkongomani Papy Tshishimbi amesema kuwa dawa ya kuwapoka ubingwa wa Ligi Kuu Bara watani wao wa jadi, Simba ni kufanya usajili bora na wa kisasa utakaoendana na hadhi ya klabu hiyo kongwe nchini.

 

Kiungo huyo tangu amejiunga na Yanga, hakufanikiwa kubeba taji lolote huku akipanga kuchukua makombe katika msimu ujao baada ya Simba kuchukua mara mbili mfululizo msimu wa 2017/18 na 2018/ 19 huku ikiwa na nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa huo kwa mara ya tatu 2019/20.

 

Yanga hivi sasa ipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 51, Azam FC nafasi ya pili na pointi 54 huku Simba wakiongoza wakiwa na pointi 71 wakati Namungo FC ikiendelea kukaa nafasi ya nne ikiwa na pointi 50.



Akizungumza na Championi Jumamosi, Tshishimbi alisema kuwa, njia rahisi ya kufanikiwa kuzuia makombe yasiende Simba ni kufanya usajili wa wachezaji wenye viwango vya juu watakaoleta upinzani kwa watani wao hao.

 

Tshishimbi alisema kuwa upo utofauti mkubwa wa usajili unaofanywa Simba na Yanga ambao wenyewe wanasajili wachezaji wakongwe ambao hutumia uzoefu kupambana uwanjani na kuamua matokeo.

 

Aliongeza kuwa kama uongozi wa Yanga ukifanya usajili mzuri kwa kuiboresha safu ya ushambuliaji, basi anaamini Simba utakuwa msimu wao wa mwisho kuchukua ubingwa.

 

“Kama kweli tunataka tuwazuie Simba wasichukue ubingwa wa ligi, basi ni lazima isukwe upya kwa maana ya kufanya usajili utakaokuwa na tija katika timu na siyo kitu kingine.

 

“Hicho ndiyo ambacho nimekiona kwangu, kwani wenzetu Simba usajili wao unazingatia wachezaji wakongwe na wenye uzoefu watakaoamua matokeo ya ushindi na siyo kitu kingine.

 

“Hivyo, viongozi wakifanyia kazi hilo katika kuelekea msimu ujao, basi ubingwa wa ligi hautaenda tena Simba na badala yake tutauchukua sisi,” alisema Tshishimbi.

Stori na Wilbert Molandi, Dar es Salaam


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad