Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, ameonya kuwa kirusi cha corona kinasambaa kwa kasi kwenye mataifa yote wanachama wa Umoja wa Ulaya, na ametoa wito wa juhudi za pamoja kuzuwia athari zake.
Mapema leo, Ubelgiji yaliko makao makuu ya Umoja wa Ulaya, imetangaza kifo cha kwanza cha mgonjwa wa COVI-19, ugonjwa unaosababishwa na kirusi hicho.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Maggie de Block, mgonjwa aliyepoteza maisha ni mzee wa miaka 90, akiwa miongoni mwa wagonjwa 297 ambao hadi sasa wamegunduliwa kuambukizwa kirusi hicho nchini Ubelgiji.
Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen, amesema kamisheni yake inatenga euro bilioni 25 kusaidia kukabiliana na athari za kiuchumi za kirusi hicho.
China inaendelea kusalia kuwa nchi yenye wagonjwa wengi zaidi ulimwenguni, ikiwa na visa 80,000 vya maambukizi na zaidi ya watu 3,000 waliopoteza maisha, huku Italia ikishika nafasi ya pili kwa kupoteza watu 631 kufikia jana.
Jumla ya watu 117,339 wamegunduliwa na ugonjwa huo duniani kote.