Umoja wa Ulaya leo umeukosoa vikali uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump wa kuzuia watu kutoka mataifa ya Ulaya kuingia nchini humo kufuatia mripuko wa virusi vya corona, ukisema kwamba ugonjwa haujali mipaka.
Pamoja na rais Trump kutangaza kusitisha safari zote kutoka Ulaya, lakini baadae maafisa wa Marekani walisema kwamba zuio hilo litawalenga tu wengi wa raia wa kigeni ambao walikuwa katika eneo la Ulaya lisilohitaji pasi za usafiri, kwa siku 14 kabla ya kuwasili Marekani.
Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel pamoja na Rais wa Halmashauri Kuu ya umoja huo, Ursula von der Leyen wamesema kwenye taarifa yao ya pamoja kwamba Umoja wa Ulaya haukubaliani na hatua hiyo ya Trump kwa kuwa imefikiwa kutokana na maamuzi ya upande mmoja, bila ya kufanyika mashauriano.
Viongozi hao wawili wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya wamesema virusi vya corona havizuiwi kuingia mahali popote na kunahitajika ushirikiano badala ya hatua za nchi moja moja. Aidha wamepinga vikali matamshi ya Trump kwamba Ulaya haichukui hatua vya kutosha kupambana na COVID-19 wakisema umoja huo wa mataifa 27 unachukua hatua kali za kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.
Katika kuonyesha mshikamano huo Von der Leyen ametuma ujumbe nchini Italia, taifa la Ulaya ambalo limeathirika pakubwa na virusi vya corona akisema wako tayari kutoa ushirikiano na kamwe hawataachwa peke yao.
''Halmashauri ya Ulaya itafanya kila liwezekanalo kuwasaidia. Mzozo huu unaathiri vibaya sekta ya afya ambayo inakabiliwa na shinikizo kufuatia kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa. Tunatakiwa kuchukua hatua za haraka na kushirikiana pamoja kuleta misaada. Ninawasiliana mara kwa mara na waziri mkuu Conte. Tunatakiwa kuisaidia kwa dharura sekta ya afya", amesema von der Leyen.
Aidha, Von der Leyen ametangaza wakfu wa uwekezaji wa Euro bilioni 7.5 wa kupambana na COVID-19 ambao amesema unatarajia kuchangisha mabilioni zaidi ya fedha.
Kando na hatua hizi za Ulaya, waziri mkuu wa Slovakia, Peter Pellegrini ametangaza hatua mpya za kupambana na kusambaa kwa virusi hivyo nchini humo ikiwa ni pamoja na kuanzisha ukaguzi wa mipakani na kuzuia watu kusafiri au kuingia Slovakia kutoka mataifa mengine, pamoja na kuzifunga shule. Slovakia imethibitisha visa 16 vya COVID-19WHO: Dunia imeingia hali ya mashaka kufuatia virusi vya Corona.
Katika hatua nyingine, mkutano wa kilele uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Machi huko Beijing, kati ya China na Umoja wa Ulaya umeahirishwa kufuatia mripuko huo. Kuahirishwa kwa mkutano huo ni pigo kubwa kwa juhudi za Ulaya za kuongeza mbinyo kwa China juu ya biashara huria.
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO hapo jana lilitangaza COVID-19 kama janga la kimataifa, lakini mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Gebreyesus, ameyahakikishia mataifa kwamba mripuko huo unadhibitika, hata katika wakati ambapo visa vikizidi kuongezeka huko Iran na Uhispania.
Iran ambayo inajikongoja kiuchumi hasa kutokana na vikwazo vya Marekani imelazimika kuomba mkopo wa dharura wa dola bilioni 5 kutoka kwa Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF kukabiliana na mripuko huo. Mkuu wa benki kuu nchini humo Abdolnasser Hemmati amesema leo kwamba amepeleka barua ya maombi kwa mkuu wa IMF, Kristalina Georgiva wiki iliyopita kuomba msaada huo.