Upulizaji dawa mabasi ya abiria kujikinga na corona wasuasuaUpulizaji dawa mabasi ya abiria kujikinga na corona wasuasua
Upulizaji dawa katika mabasi yaendayo mikoani katika stendi ya kuu ya mabasi ya Ubungo jijini Dar es Salaam (UBT) ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona bado haujaanza.
Katika mkakati wa kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo kwenye vyombo vya usafiri, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) iliwataka wamiliki wa mabasi wanyunyizie dawa za kuua virusi katika mabasi yao kila mwisho wa safari.
Mwananchi imefika kituoni hapo leo Jumamosi Machi 21, 2020 na kuzungumza na baadhi ya madereva waliosema kuwa jambo hilo halijaanza kutekelezwa.
Dereva wa kampuni ya mabasi ya Simba Mtoto, Gumbo Juma amesema upiliziaji huo katika stendi hiyo haujaanza, kudai kuwa mkoani Tanga tayari wameanza.
"Stendi ya Tanga asubuhi gari huwa inapuliziwa dawa na nyingine tunapewa kwa ajili ya kuondoka nayo, ila changamoto kubwa ni elimu kwa abiria,” amesema Juma.
Dereva mwingine wa kampuni ya mabasi ya Moud, Salim Four amesema pamoja na upulizaji huo wa dawa elimu inatakiwa kuendelea kutolewa.
“Hata kama dawa zitapulizwa ninachokiona ni elimu kwa abiria maana mtu akishanawa mikono baada ya kuingia stendi anajiona amemaliza,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliad Ngewe amesema kuchelewa kuanza kwa upilzaji huo wa dawa unatokana na upatikanaji wake.
“Pale Ubungo kuna mabasi mengi na hili zoezi linategea na namna ya upatikanaji wa dawa lakini tunaendelea na jitihada zakuhakikisha tunafanikiwa,” amesema Ngewe.
Mmoja wa abiria aliyezungumza na Mwananchi, John Mndeme amesema Serikali inatakiwa kutoa elimu zaidi hasa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu.