Utafiti Mpya wa Kisayansi wa Covid19 – Msaada Mkubwa wa Kujikinga na Kuzuia Maambukizi kwa Wengine



Watafiti wa vyuo vikuu na taasisi kadhaa za utafiti wa magonjwa ya mlipuko nchini Marekani, wamechapisha utafiti mpya wa kimaabara unaotoa mwanga mkubwa wa namna virusi wa Covid19 wanavyasambaa na kuambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine (UKO HAPA). Kwa kuwa sio kila mtu anasoma machapisho ya kisayansi, ninaomba nijaribu kutoa ufupisho wa matokeo ya utafiti huu na tafsiri yake ya namna yanatusaidia katika kupambana na mlipuko wa Covid19.

Kwa kuanzia, ili kuelewa utafiti huu, chukulia unapuliza Doom (spray) kuua wadudu au unapuliza spray ya kuleta harufu nzuri kwenye chumba/nyumba (air refresher). Tunapopuliza spray hizi hutoa matone madogomadogo kama ya maji yanayobaki hewani au kwenye uso wa kitu ulichopulizia kwa muda kufanya kazi kusudiwa (kuua wadudu au kuleta harufu nzuri). Kwa lugha ya kikoloni matone haya huitwa “Aerosols” ila kwa malengo ya ufafanuzi huu sisi tuite tu kizaramo kwamba ni matone.

Mtu anapokohoa au kupiga chafya matone (mate, makohozi au kamasi) hubaki ama hewani au kwenye kitu yalipoangukia kwa muda na kua chanzo cha maambukizi ya Covid19. Utafiti huu mpya umegundua yafuatayo kuhusu uwezo wa virusi wanasababisha Covid19 kuendelea kuwa hai na ambukizi pale matoke yanapokua hewani (aerosol transmission) au yanapoangukia kwenye uso wa kitu (surface/fomite transmission):
Matone ya Covid19 yakiwa ndani ya nyumba (closed doors), virusi hao wanabaki hewani wakiwa hai na ambukizi kwa hadi masaa 3.

Matone yakiangukia kwenye kitu cha plastiski (polypropylene) au chuma (stainless steel), virusi wanakua hai na ambukizi kwa hadi masaa 72 (siku 3).
Matone yakiangukia kwenye kitu kilichotengenezwa kwa mbao (cardboard), virusi wanakua hai na ambukizi hadi masaa 24 (siku moja).
Matone yakiangukia kwenye kitu kilichotengenezwa kwa shaba (copper) virusi wanakua hai na uwezo wa kuambukiza kwa hadi masaa 4.

Popote matone yanapokuwepo, virusi wa Covid19 hawafi mara moja kama vile mtu anapokata roho muda unapofika. Virusi hawa hukata roho kwa mfumo unajulikana kisayansi kama “half-life decay” (sina neno la kizaramo). Ila kwa kifupi, wanakufa nusunusu au wanaoza hadi wanapoangamia kabisa. Kwa mfano, kwenye uso wa plastiki virusi wanakufa au kaoza nusunusu kila baada ya masaa 6 dakika 48 (half-life time is 6.8 hours) hadi siku ya 3 kukamilika fungu la mwisho la virusi wanakua wamekufa.

Nini maana ya half-life decay (kufa/kuoza nusunusu)?
Ukitaka kuelewa dhana ya kufa nusunusu chukulia virusi wa Covid19 ni chungwa. Sasa chukua chungwa kaa nalo kwa masaa 6 dakika 48 kisha likate nusu. Tupa nusu moja (imekufa/ imeoza) ubaki na moja (hai). Baada ya muda mwingine kama huohuo ile nusu hai uikate tena nusu (unabaki na robo hai) kisha tupa robo nyingine (imekufa/imeoza). Endelea hivyohivyo hadi kipande cha mwisho ushindwe kabisa kukikata kwa uwembamba wake na hivyo kukitupa. Ukifikia hatua hiyo utakua umefikisha siku 3 (yaani virusi wote wamekufa).

Nini tafsiri ya utafiti huu na unatusidiaje kupambana Covid19
Utafiti huu unatupa mwanga zaidi kuhusu maambukizi ya Covid19 na kutueleza ni kwa nini unaambukiza kwa haraka. Pia unatueleza ni kwa nini imekua vigumu kudhibiti maambukizi ya Covid19. Kwa mfano, tukipanda basi pale Kimara Mwisho tunaelekea posta, kisha kukawa na mtu ambaye ana Covid19 bila kujijua akakohoa au kupiga chafya (mara moja tu), basi kuna uwezekano mkubwa watu wengi watagongana na matone hata wale watakaopanda baadaye pale Ubungo au Manzese. Ikitokea hilo wanaweza kuambukizwa (usitishike ni mfano tu). Pia watakaoshika viti, chuma au eneo lolote la basi ambapo matoke yamedondokea, wataondoka na virusi mikononi na watakapojishika usoni basi watakua wamewakaribisha kupia kinywa, macho au puani.

Hivyo basi, utafiti huu unatuonesha kwa nini ni muhim sana mtu mwenye Covid19 anapokua karibu na watu wengine avae mask. Pia, kwa kuwa hatufahamiani nani anao, basi ni vema tunapoongea tuwe na umbali wa kadiri ili matone yanayotoka mtu anapoongea (na wengine kama mimi huwa yanatoka kwelikweli) yasikufikie.

Kwenye hili, niwasisitize vongozi wetu wanapokua wanaongea na vyombo vya habari wakiambatana na timu yao ya wataalamu na viongozi wenzao, wasikaribiane sana. Hadi sasa viongozi wa nchi kadhaa waliokua ndio wasemaji wakuu wa ugonjwa huu, wameathirika na wengine wamelala mauti na huenda waliambukizwa kwa njia hii.

Utafiti huu unaendelea kuthibitisha ni kwa nini kujitenga (social distancing and isolation) kwa mtu aliyeathirika ni njia muhimu sana ya kudhibiti maambukizi kwa wengine. Sio tu kwamba baada ya siku 7 hadi 14 atakua kapona kama hana hali mbaya ya kutibiwa hospitali, bali chumba au nyumba atakayokua amejitenga haitakua na virusi kwa kuwa muda wao wa kuendelea kuwa hai utakua umeshapita kwa kifo cha kinusunusu.

Utafiti huu unaendelea kutukumbusha umuhim wa kutoshikashika maeneo yoyote ambayo watu wengine wanashika kama vile milango ya nyumba na magari, chooni, ngazi, viti, reli za kwenye ngazi, nk. Hii ni ngumu sana kuepuka lakini inapowezekana jitahidi usishike maana huenda kuna kafungu ka vikorona ndio kwanza vimekufa robo tatu vimebaki robo moja na utaondoka nao.

Utafiti huu unatusisitiza umuhim wa kujitahidi kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka kila unaposhika mahali wanaposhika watu wengine au kutumia kitu ambacho kimetumiwa na watu wengine. Baada ya kunawa jitahidi kujifuta na tissue na kuitupa au kutumia taulo safi ambayo una hakika ni wewe mwenyewe unaishika. Ikishindikana usijifute baada ya kunawa (hata kwa nguo ulizovaa). Kung'uta mikono iache ikauke.

Mwisho
Ninaomba unisamehe kwa lugha ya kizaramo isiyo rasmi niliyotumia hapa. Ni ngumu sana kutafisiri maandiko ya kisayansi yaliyo katika lugha ya kikoloni kwenda kwenye lugha ya kizaramo na ukaeleweka hasa unapokua kwenye kiwewe cha korona. Bado ninajifunza.

Imeandikwa na Mathew Mndeme (mmtogolani@gmail.com)
Mwanasayansi/Mtafiti wa mifumo ya digitali kwenye ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Unafaa kuwa Mwalimu. Asante, umetusaidia sana

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad