Wabunge Chadema wasimulia walivyopigwa na askari Magereza




Wabunge wawili wa Chadema, Halima Mdee na Ester Bulaya wamesimulia jinsi walivyopigwa na askari Magereza walipokwenda katika Gereza la Segerea kumpokea mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyekuwa akitoka jela baada ya kukamilisha taratibu za kulipa faini ya Sh70 milioni.

Wakizungumza jana na Mwananchi katika Hospitali ya Aga Khan walikolazwa, wabunge hao wa Kawe na Bunda wameeleza tangu walipofika katika gereza hilo, walivyoshushwa kwenye magari, kupigwa na kisha kupelekwa Kituo cha Polisi Stakishari walikotoa maelezo na kuachiwa kwa dhamana.

Wakati Mdee akisema amevunjwa mkono wake wa kulia, Bulaya alisema ameelezwa kuwa pingili za mgongo zimetikisika kutokana na kukanyagwa huku Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ambaye pia alikuwa na wabunge hao akieleza hali ilivyokuwa.

Mdee, Bulaya na Jacob pamoja na diwani wa Tabata, Patrick Assenga na Katibu wa Chadema Dar es Salaam Kuu, Henry Kileo ni kati ya watu 27waliokamatwa katika gereza hilo walikoenda kumchukua Mbowe.

Wengine ni Mbunge wa Viti Maalum, Jesca Kishoa na mjumbe wa baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Hadija Mwago.

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Magereza SSP, Amina Kavirondo alisema, “hakuna mtu aliyepigwa, kilichofanyika walikuwa wakizuiwa kutoingia eneo la Magereza.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad