Wafungwa 23 Wafariki Dunia kwa Jaribio la Kutoroka Gerezani Kisa Corona
0
March 24, 2020
Wafungwa 23 wamefariki dunia baada ya kutokea mkanyagano uliosababishwa na hofu ya kuenea kwa virusi vya corona katika gereza moja nchini Colombia.
Vurugu hizo zilitokea usiku wa kuamkia jana katika gereza lenye mrundikano wa wafungwa lililopo katika mji mkuu wa Bogota, Colombia baada ya uvumi kusambaa kwamba virusi vya corona vimeingizwa katika gereza hilo.
Hata hivyo, Waziri wa Sheria, Margarita Cabello alisema vitendo hivyo ni njama za baadhi ya wafungwa kutaka kutoroka gerezani.
Waziri Cabello alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba mpango huo uliratibiwa na wafungwa katika na magereza karibu 13 nchi nzima.
Waziri huyo alisema taarifa zinazosambazwa na watetezi wa haki za binadamu kwamba vurugu hizo zimetokana na mazingira machafu gerezani hazina ukweli wowote.
Katika hatua nyingine, daktari mmoja amefariki dunia nchini Ufaransa kutokana na virusi vya corona.
Waziri wa Afya wa Ufaransa, Olivier Veran alisema kuwa kifo cha daktari huyo aliyekuwa akiwahudumia wagonjwa wa corona ni cha kwanza kurekodiwa nchini humo.
Hata hivyo, waziri huyo hakuwa tayari kueleza zaidi kuhusu daktari huyo.
“Taarifa zake zinahifadhiwa kwa sababu za kitabibu na kuheshimu matakwa ya familia ya daktari huyo,” alisema Waziri Veran.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, daktari huyo alikuwa akifanya kazi katika Hospitali ya Compiegne.
Tags