Katika hali ambayo hakuna dawa mjarabu ya kutibu ugonjwa wa Corona iliyotangazwa rasmi au kuidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), lakini waganga wa kienyeji nchini Tunisia wameendelea kupata faida kubwa kutokana na mauzo ya mitishamba na dawa za kiasili wanazodai kuwa zinatibu Corona.
Katika mji mkuu Tunis, wananchi wameendelea kumiminika katika soka la jadi la Souk el-Blat lenye waganga wa kienyeji kutafuta kinga au tiba ya Corona.
Mbali na kwenda kwa waganga wa kienyeji, baadhi ya Watunisia wanatumia vitunguu saumu kujikinga dhidi ya Corona, jambo ambalo limefanya bei ya bidhaa hiyo iongozeke, na hivi sasa inauzwa dinari 25 (yuro 8) kwa kilo.
Dakta Hedi Oueslati, Mkurugenzi wa Afya ya Umma wa Tunisia amewatahadharisha wananchi dhidi ya kwenda kwa waganga hao wa kienyeji kutafuta tiba ya Corona au kutumia mimea inayodaiwa kutibu Corona.
Dakta Oueslati ambaye pia ni mwanafamasia amefafanua kwa kusema, "nafahamu hofu ya watu iliyowafanya warejee katika tiba asilia, lakini hivi sasa hakuna dawa wala mmea wa muujiza unaotibu Corona."