KWA mara ya pili ya Serikali imetoa fursa kwa wanafunzi waliofaulu kidato cha nne mwaka 2019 na wanaotegemea kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo kwa mwaka 2020 kubadilisha Tahasusi(Combination).
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Miko na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Mhe.Jafo amesema kuwa Fursa hii itawawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya Kidato cha Nne 2019 yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania, NECTA.
“Huu ni mwaka wa pili Wanafunzi watakuwa na uwezo wa kubadili machaguo au kuchagua kutoka Kidato cha Tano kwenda Chuo au Chuo kwenda Kidato cha Tano kwa kadiri ya mahitaji yake na jinsi alivyofaulu mitihani yake” amesema Jafo.
Waziri amesisitiza kuwa wanafunzi walikuwa wanajaza Fomu za F4-Selform kabla ya kufanya mitihani sasa matokeo huweza kuja tofauti na vile alivyojaza lakini mwanafunzi huyo amefaulu.
Aidha Waziri ameongeza kuwa Ofisi yake imetoa fursa hii kwa wahitimu kubadili machaguo yao ili kutoa mwanya zaidi kwa mwanafunzi kusoma fani au Tahsusi itakayomwandaa kuwa na mtaalam fulani katika maisha yake ya baadaye kwa namna ambayo anatamani yeye mwenyewe au kwa kushauriwa na wazazi au walezi wake.
Hata hivyo Jafo amesema kuwa wanafunzi hao watabadili kwa njia ya mtandao kadri watakavyotaka na baada ya kufanya marekebisho hayo kanzidata hiyo itatumika kuwapanga kwa ajili ya kidato cha tano na kozi za vyuo.
“Wanafunzi watumie anuani ya www.selform.tamisemi.go.tz na maelekezo ya jinsi ya kufanya mabadiliko yanapatikana kwenye Youtube video iliyoko kwenye tovuti ya Tamisemi ya www.tamisemi.go.tz,” amesema Jafo
Mhe.Jafo amesema kuwa Miaka ya nyuma tukishafanya selection (kuchagua wanafunzi) wanafunzi na wazazi walikuwa wanakuja tamisemi kutaka kubadili Tahasusi au kozi aliyoomba kujiunga na chuo, lakini sasa tumetoa fursa hiyo wafanye hivyo.
Jafo amesema endapo mwanafunzi hataomba kubadilishiwa tahasusi au kozi alizoomba, basi taarifa zake za awali alizojaza akiwa shule ndizo zitakazotumika kuwapanga katika shule na vyuo.
Waziri Jafo amesema kuwa zoezi hili la kubadilisha Tahsusi litafanyika kuanzia leo Machi 25 hadi tarehe 19/04/2020.