Afisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara amefika Makao Makuu ya klabu ya Yanga kwa ajili ya kurejesha pesa za matibabu alizochangiwa na mashabiki wa klabu hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Manara amesema kuwa ameamua kubadilisha uamuzi wake baada ya kukutana na wazee wa Yanga Makao Makuu ya klabu na kumshauri kuwa asitishe mpango wake kwakuwa wao ni watani wa jadi kwa muda mrefu.
"Nilikwenda mwenyewe mchana huu klabuni Yanga,bahati mbaya sana sikuwakuta viongozi wa klabu, wazee niliowakuta nje baada ya kuwaeleza nimekuja kukabidhi pesa za masimango walinisihi sana nisifanye hivyo na wakaniambia yule ni mgeni hapa mjini na hajui tamaduni zetu na kuniomba nisirejeshe hata thumni", amesema Manara.
"Nimefundishwa kuwatii wazee, na ntarejea kwa Wanasimba walionikabidhi pesa zao, busara itawashauri tupeleke hospitali kwa wagonjwa wasiojiweza, ikiwapendeza tutafanya hvyo", ameongeza.
Hatua hiyo imekuja baada ya maoni ya mmoja wa watu maarufu ndani ya klabu ya Yanga, maoni ambayo Manara amesema hayakumpendeza yanayohusu pesa ambazo aliwahi kuchangiwa na mashabiki wa Yanga kwa ajili ya matibabu yake.
Joto la mchezo wa mahasimu hao linazidi kupanda, ambapo mchezo wao unatarajiwa kupigwa Machi 8, 2020 katika Uwanja wa Taifa, huku Yanga wakiwa wenyeji.