Waziri Mkuu Akanusha Taarifa Ya Shule, Vyuo Kufunguliwa Kesho



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao kwamba vyuo na shule vitafunguliwa kesho siyo za kweli.

“Hizo taarifa ni za upotoshaji, zipuuzwe,” amesema leo usiku (Jumanne, Machi 24, 2020).

Taarifa hiyo ambayo haioneshi chanzo chake kama ni ya kwenye televisheni au kwenye blog, imeunganisha kauli ya TAMISEMI na kuweka picha ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikionesha kwamba vyuo na shule vitafunguliwa Jumatano bila kuonesha ni Jumatano ipi.

Jumanne iliyopita (Machi 17, 2020), Waziri Mkuu alitangaza kuwa shule zote za awali, msingi na sekondari zitafungwa kwa siku 30 ili kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19).

Na siku iliyofuata (Jumatano, Machi 18, 2020), Waziri Mkuu alitangaza kwamba vyuo vyote vya elimu ya kati na vya elimu ya juu vitafungwa kwa muda wa siku 30 ili kuondoa msongamano katika maeneo hayo na kuweza kujikinga na virusi vya corona.

Alisema mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo ya lazima imesitishwa kuanzia siku hiyo ikiwemo shughuli za michezo, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, mahafali na shughuli nyingine za kijamii.

Alizitaka wizara na taasisi zisitishe semina, warsha, makongamano na mikutano yote hapa nchini ambayo inahusisha washiriki toka nchi zenye maambukizi makubwa. “Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye maambukizi makubwa, wanashauriwa wasitishe safari hizo,” alisisitiza.

Ili kudhibiti ugonjwa huo, Serikali pia ilisitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu ikiwemo Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Ligi Daraja la Pili (SDL) na aina nyngine.

Ugonjwa huo uliingia nchini baada ya Mtanzania mwenye miaka 46 aliyesafiri kwenda nchi za Ubeligiji, Sweden na Denmark hivi karibuni, kupimwa na kuthibitika kuwa na virusi vya Corona (COVID-19).

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad