BONDIA Mike ‘Iron’ Tyson hatimaye amejutia kitendo chake cha kufuga na kuishi nyumba moja na chui milia (tiger) wawili hatari miaka hiyo akiwa bingwa wa dunia.
Tyson (53) amefichua kuwa alikuwa anafanya makosa makubwa kuishi na wanyama hao wakali katika makazi yake yaliyokuwa Las Vegas na kufikia hatua ya kuishi nao kikawaida kwa kuwaamini asilimia 100 ikiwemo kulala nao na kucheza kitu ambacho hakikuwa sahihi kwani hawatakiwi kuaminiwa kiasi hicho.
Matokeo yake yalimfanya alipe faini ya dola 250,000 kwa chui milia wake kumng’ata mkono mwanamke aliyekuwa akipita karibu naye jambo ambalo linamthibitishia makosa yake makubwa aliyoyafanya ambayo anakiri alikuwa hajielewi kwa kitendo cha kufuga wanyama hao hatari na kwamba binafsi ameelewa madhara ambayo hayapaswi kufanywa na mtu mwingine.
Baada ya kufungwa jela mwaka 1992 na kutumikia miaka sita kwa tuhuma za ubakaji, Tyson alinunua chui milia hao akifuata ushauri aliouita mbaya wa mtu aliyemwamini na aliyemuuzia gari aliyemshauri pia ishu ya kumiliki wanyama hao hatari na ndipo alipoamua kununua na baadaye kubaki na mmojawapo.
Ni baada ya miaka 16 ya kuishi na chui huyo alipolazimishwa kumuuza baada ya kumng’ata mwanamke huyo ambapo mwanzoni mwa mwaka huu alikiri kuwa na mapenzi makubwa na mnyama huyo wakati alipokuwa anammiliki akiwa mdogo hadi ilipolazimika aachane naye.