MASHABIKI wa Yanga na Simba hapa nchini wana hamu kubwa sana ya kuona usajili wa wachezaji wao wa zamani ukitimia na msimu ujao kuwaona tena mastaa wao waliotesa msimu uliopita kabla ya kusepa.
Yanga wanatamani kumuona tena Heritier Makambo akiwa na jezi ya timu hiyo huku akiwajaza kwa staili yake ya kushangilia anapofunga bao, lakini pia Simba wakitaka Emmanuel Okwi arudi kikosini kwao kuja kuungana tena na Meddie Kagere na John Bocco kuendeleza moto kama msimu uliopita ambao walifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Sasa wakati kukiwa na kiu hiyo ya mashabiki wa Yanga na Simba, Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeingilia kati juu ya masuala ya usajili wote kwa timu hizo na zingine duniani kote.
Fifa baada ya kuona janga la Corona likiendelea kuutesa ulimwengu huku ligi mbalimbali duniani zikisimama na haijulikani zitaendelea lini kumaliza msimu, imesema kwamba suala la usajili litategemea na msimu wa ligi husika utamalizika lini.
Katika taarifa iliyotoka jana, inasema kwamba, wachezaji ambao mikataba yao ilitarajiwa kumalizika Juni au Julai, mwaka huu, hawataondoka katika timu zao hadi wamalize msimu, ndipo wataruhusiwa kuondoka. Pia wataendelea kulipwa kama kawaida hadi watakapomaliza msimu hata kama mikataba yao inaonyesha inamalizika nje ya muda wa kawaida.
Uwepo wa Virusi vya Corona ambavyo vinasababisha ugonjwa wa Covid-19, imeleta hofu kwamba kuna baadhi ya ligi msimu huu zikamalizika Juni, Julai au Agosti tofauti na ilivyo kawaida kumalizika Mei.
Ligi Kuu Bara awali ilitarajiwa kumalizika Mei, mwaka huu, lakini baada ya kusimama kutokana na janga la Corona, sasa italazimika kuendelea Juni 30, mwaka huu, hivyo kuna uwezekano ikamalizika Agosti, mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo, nyota wote wa Simba, Yanga, Azam na timu nyinginezo hapa nchini ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika Juni, mwaka huu, hawataruhusiwa kuondoka hadi wamalize msimu iwe Juni au Julai. Lakini pia, wale wapya wanaotakiwa na timu za Simba na Yanga na nyinginezo, watasubiri hadi ligi zao zimalizike ndipo watue Bongo.
Baadhi ya nyota ambao wanahusishwa na Yanga kwa ajili ya msimu ujao ni Makambo (Horoya, Guinea), Tuisila Kisinda (AS Vita, DR Congo), Jimmy Ukonde (UD Songo, Msumbiji), Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ (Azam), Reliants Lusajo (Namungo) na Said Ndemla (Simba).
Wale wanaotajwa kutakiwa na Simba ni Okwi (Al Ittihad Alexandria, Misri), Justin Shonga (Orlando Pirates, Afrika Kusini), Yakub Mohamed (Azam) na Bakari Mwamnyeto (Coastal Union).
Lakini pia, kuna nyota wa Yanga ambao wanamaliza mikataba yao, miongoni mwao ni Juma Abdul, Mrisho Ngassa, Kelvin Yondani, Papy Tshishimbi, David Molinga, Jaffery Mohammed, Said Makapu na Mohammed Banka. Simba wanaomaliza mikataba baadhi ni Sharaf Shiboub, Pascal Wawa, Hassan Dilunga, Yusuf Mlipili na Mzamiru Yassin.