GSM yatangaza Kurejea Yanga kwa Kishindo Baada ya Kumaliza Tofauti zao
0
April 08, 2020
WADHAMINI wa Yanga, Kampuni ya GSM wamerudi kwa kishindo baada ya kumaliza tofauti zao ambazo ziliwafanya hivi karibuni watangaze kujitoa kuisaidia klabu hiyo kwenye mambo mengine nje ya mkataba wao.
Mmoja wa Wakurugenzi wa GSM, Hersi Said amesema kuwa jambo la kwanza watakaloanza nalo ni kuhakikisha mchakato wa mabadiliko unaanza mwezi ujao, Mei kama walivyokubaliana na Mwenyekiti Dk. Mshindo Msola.
Hersi amesema wakati wanaendelea na mchakato huo jambo la pili wamejipanga kuitengeneza Yanga imara tofauti na hii ya sasa ambayo imeshindwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo kwa maana ya kufanya usajili wa wachezaji waliokuwa bora na viwango vya juu.
"Tutaanza na mabadiliko ya mchakato huo mwezi ujao, upande wetu GSM tumekubali kudhamini mchakato wote mpaka unakamilika kwa kufanya mambo ya msingi kama kuleta mtaalamu na kutengeneza timu ya watu sahihi kusimamia mchakato mzima,"
"Baada ya kuwepo na hali ya sitofahamu kati yetu na viongozi wa Yanga, kama GSM tunatoa tamko rasmi tunaendelea kuwepo hapa kama mkataba wetu unavyoonyesha na tutatimiza majukumu ya kimkataba yote na kufanya mambo mengi ya kimsingi kama ilivyokuwa hapo awali,"
"Tunaelekea kuijenga Yanga kuhakikisha inafanya vyema kwa kufanya usajili wa wachezaji wa maana ambao watakuwa na uwezo kulingana na mahitaji ya timu yetu na tutawatunza katika mazingira sahihi ili tuweze kufanikiwa malengo yetu ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu ujao," amesema Hersi.
Kwa upande wa Msolla amesema suala la mabadiliko haliepukiki na tayari wameweka mipango kamili ya kulianzisha jambo hilo ambalo wamelipanga kuanza mchakato wake mwezi ujao.
"Tutaunda kamati nyingine ya pili ambayo itakuwa kamati ndogo ya masuala ya kikatiba ambayo tutaipeleka kwenye matawi ya nchi nzima ili nao wasome na kuelewa jambo gani wanakwenda kulifanya katika klabu yao na kutoa idhini kuwa lifanyike kwa mfumo upi,"
"Suala la mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu ni moja ya kipaumbele changu, pia uongozi una dhamira ya kuhakikisha msimu ujao tunatwaa ubingwa," amesema Msolla
Tags