HISIA ZANGU : Wachezaji Wapo Katika Mikataba Kama ya Kina Carl Peters
0
April 07, 2020
NIMEONA mikataba ya baadhi ya wachezaji mastaa hapa nchini. Inachekesha. Kwanza kabisa haiwalindi wachezaji. Ni mikataba ya kina Carl Peters enzi za ukoloni. Leo nimekuja kupiga domo kuwakumbusha wachezaji mambo muhimu wakati wanaingiza mikataba.
Mikataba ya wachezaji haipaswi kufanana. Mkataba wa Aishi Manula sio lazima ufanane na wa Shomari Kapombe hata kama wote wapo katika klabu moja. Mkataba wa Ditram Nchimbi sio lazima ufanane na wa Fei Toto ingawa wote wanachezea Yanga. Haya ni mambo ya kizamani. Kila mwanadamu ana mahitaji yake kulingana na jinsi anavyoyachukulia maisha yake.
Kwanza kabisa hakikisha una vipengele vyako katika mkataba. Wachezaji wengi wanatumikia vipengele vya klabu tu. Vya kwao viko wapi? Sielewi. Mara nyingi mkataba ni wa klabu tu. Sio wa pande zote mbili. Kwanini Mwanasheria wako hakukutana na yule wa klabu kujadili vipengele unavyotaka?
Mazungumzo ya mkataba baina ya mchezaji na klabu barani Ulaya huwa yanachukua muda mrefu kwa sababu pande mbili zinajaribu kuingiza vipengele vyenye maslahi baina yao. Kila mmoja anajaribu kuangalia maslahi yake. Sio suala la pesa tu, bali jinsi yatakavyokwenda.
Kwa mfano, Dennis Bergkamp aliingiza katika mkataba wake kuwa hatasafiri kwa ndege akiwa na klabu yake ya Arsenal. Hii ina maana kwamba Arsenal walikuwa hawamlazimishi Bergkamp kupanda ndege. Haijalishi timu ilikuwa inakwenda kucheza wapi.
Wengi wanaposikia Bergkamp hapandi ndege wanaamini kwamba alisema tu kwa mdomo au kwa kujisikia kwake. Hapana, aliweka kipengele katika mkataba wake ili klabu isimlazimishe. Kila kitu lazima kikae katika maandishi.
Lakini pia mchezaji anaweza kuandika katika mkataba wake kwamba anahitaji ongezeko la shilingi laki tano katika mshahara wake kama timu ikichukua ubingwa huku yeye akiwa amecheza asilimia 80 ya mechi zote. Wenzetu wanaweka haya katika mkataba.
Mchezaji pia anaweza kuingiza kipengele ambacho kinamtaka awe analipwa zaidi klabuni kama akifunga mabao 25 ndani ya msimu mmoja. Ni suala la kujivunia uwezo wako tu. Ni suala la kutaka mahitaji yako yatimizwe.
Hapo hapo kuna kile kipengele kikubwa zaidi. Mchezaji lazima aangalie thamani yake halisi na kuweka kipengele kwamba endapo kuna timu imefika dau la kiasi fulani cha pesa basi lazima auzwe kama akihitaji kuondoka.
Kuwa na mkataba sio sababu ya kutouzwa. Rais wa zamani wa Juventus, Luciano Moggi aliwahi kusema ‘Hakuna mchezaji asiyeuzwa duniani, inategemea tu na dau lako’. Wakati mwingine Tanzania inachekesha unaposikia klabu inajinasibu kwamba mchezaji wao hauzwi kwa sababu ana mkataba. Hii sio sababu ya msingi.
Wachezaji lazima wawe na vipengele hivi. Kwamba kama kuna timu inataka kumnunua na imefikia dau la dola 20,000 basi auzwe. Tanzania wachezaji wamegeuzwa watumwa na wakati umefika sasa kwa klabu kuacha kugeuza wachezaji kuwa watumwa.
Wachezaji pia waingize vipengele vya kuwawezesha kuondoka katika timu kama hachezeshwi kwa asilimia fulani ya mechi. Tanzania kuna wachezaji wa wale watani wa Kariakoo huwa wanatamaniwa sana. Unakuta mchezaji hatumiki lakini akitaka kwenda kwa watani basi anabaniwa. Kisa? Ana mkataba. Inakera.
Lakini sio mbaya wachezaji wetu wakiacha tabia ya kuona aibu kuhusu suala lao la kutojua lugha ya Kiingereza. Kwanini mikataba iandikwe katika lugha ambayo hawaifahamu vema? Kwanini mikataba isikae katika lugha ya Kiswahili? Wachezaji wetu waombe mikataba iandikwe katika lugha ya Kiswahili.
Lakini hapo hapo wachezaji wetu wakumbuke kusaini kila ukurasa wa mkataba. Kuna wajanja huwa wananyofoa kurasa na kuweka nyingine ambazo zina vipengele tofauti. Ujanja huu uliwahi kutumika kwa mchezaji mmoja mkubwa kwa sasa wakati alipoibuka katika timu fulani ya vijana ya klabu kubwa.
Mchezaji alisaini mkataba wa miaka miwili. Akachukua pesa yake. kiongozi mmoja mjanja akachomoa ukurasa unaoonyesha kwamba mchezaji kasaini miaka miwili akachapisha ukurasa mwingine unaoonyesha mchezaji amesaini mkataba wa miaka minne.
Pamoja na yote hawa wachezaji wakumbuke kwamba nje ya mpira wanaweza kuwa na majina makubwa ambayo yatawapa haki ya kufanya matangazo ya biashara mbalimbali. Wachezaji waandike katika mikataba yao kwamba wataweza kuingia katika dili binafsi bila ya kuguswa na klabu.
Kwa mfano, kuna wachezaji huwa wanafanya matangazo na kampuni ya Nike lakini timu zao zinadhaminiwa na Adidas. Kwa Tanzania mambo haya hayajatokea lakini siku yakitokea unaweza kusikia kwamba klabu inamkataza mchezaji kufanya matangazo.
Tuuvute mfano wa karibu. Kwa mfano, Simba inadhaminiwa na Mohamed Dewji ambaye ana kampuni zina bidhaa mbalimbali kama vile maji ya kunywa. Vipi kama Aishi Manula akitakiwa na kampuni ya Azam kwa ajili ya kutangaza maji? Mkataba wake na Simba unasemaje?
Wachezaji wetu wasikimbilie kusaini mikataba ambayo haiwaweki huru. Suala la mikataba limekuwa muhimu kila uchao na wakati umefika kila mchezaji kupitia mwanasheria wake au meneja wake akawa makini na masuala ya mikataba ya kikoloni.
Wachezaji wasihofie kuonekana wakorofi. Wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi kwa sababu mchezo wa soka ni kazi ya muda mfupi kwa wachezaji. Mara nyingi klabu zinavutia upande wao na wachezaji wanapaswa kuvutia upande wao. Maslahi lazima yakutane katikati.
Wakati mwingine kila upande unakuwa na haraka bila ya sababu. Kwa mfano, hata klabu ina haki ya kuweka kipengele cha kumuacha bure bila ya kumlipa chochote mchezaji ambaye kiwango chake hakiridhishwi kama Yikpe. Ni suala tu la kuandikishiana tu mapema.
Tags