Serikali imehamisha wagonjwa wote waliokuwa wakipata huduma za afya katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dar es Salaam, Amana iliyopo Manispaa ya Ilala, ili kuanza kutekeleza jukumu la kutumia hospitali hiyo kutoa huduma za afya kwa wagonjwa wa Corona (COVID – 19).
Akizungumza na Watumishi wa hospitali hiyo mara baada ya kutembelea majengo yatakayotumika kuwalaza wagonjwa wa Corona (COVID-19), Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Zainab Chaula amesema wagonjwa waliokuwa wanapata huduma katika hospitali hiyo wamehamishiwa katika hospitali nyingine za Serikali jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali imetoa kiasi cha Shilingi Milioni Mia Mbili (200m/-=) kwa ajili ya ukarabati mdogo wa baadhi ya majengo ya hospitali hiyo. Dkt. Chaula amewataka watumishi wa sekta ya afya kukumbuka kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo kwa kuvaa vifaa vya kujikinga na maambukizi wakati wa kuwahudumia wagonjwa
wa COVID-19 hospitalini hapo.
Amewakumbusha watumishi wa sekta ya afya nchini kutimiza wajibu wao katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Corona huku wakizingatia kiapo cha utii wa majukumu yao ya utoaji huduma za afya kwa wagonjwa.
Amesema Serikali ipo tayari kuwezesha huduma za afya kutolewa kikamilifu kwa wagonjwa wa Corona nchini na kuwa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanya juhudi mbali mbali za kupunguza maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo nchini zilizosababisha kuwa na wagonjwa wachache hadi sasa ukilinganisha na nchi nyingine.
Akizungumzia uamuzi huo wa Serikali Ijumaa wiki hii, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi Ummy Mwalimu alisema Serikali imeelekeza Hospitali ya Taifa Muhimbili kuacha kupokea wagonjwa wenye dalili za virusi vya Corona (CODIV-19) ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma za kibingwa na huduma bobezi kwa wagonjwa wa magonjwa mengine nchini.
Alisema, badala yake Serikali imeamua kutumia Hospitali ya Amana kama kituo maalum cha matibabu ya ugonjwa wa CODIV-19. Wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wanaohitaji kupata huduma za matibabu ya magonjwa mengine katika Hospitali ya Amana wanatakiwa kutumia hospitali nyingine zilizopo mkoani humo.