Hukumu Dhidi Yangu: Shukrani Kwa Watanzania – Maxence Melo


Wakuu,

Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru watanzania kwa ujumla na hasa watumiaji wa mitandao ya kijamii na kwa namna ya kipekee wanachama wa JamiiForums kwa support ambayo tumekuwa tukiipata toka kwenu tangu mwanzo wa kesi hii hadi mwisho wake.

Hukumu hii ya kesi namba 456 ya mwaka 2016 imetolewa baada ya kuahirishwa mara 5 kwa sababu mbalimbali tangu Novemba 26, 2019. Hatimaye imetolewa na wote naamini mmesikia kuwa imeamriwa nilipe TZS Milioni 3.

Ingawa hakimu Thomas Simba amesema kuwa hakukuwa na ulazima wa kuwapa Data walizotaka Polisi, amesema kosa langu ni kuwa nilikiri kuwa Mkurugenzi wa Kampuni na kuwa mwanzilishi wa JamiiForums; hivyo akahitimisha kuwa nilijua wazi Polisi walikuwa wanafanya uchunguzi na niliwachelewesha kwa kukusudia na sikuwambia kuwa data hizo sina.

Nisingependa kuingia kwa undani juu ya Hukumu ya Shauri hili lakini nipende kuwafahamisha kuwa baada ya hukumu, tayari leo hii mawakili wangu wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala wamewasilisha notisi ya kukata rufaa na imepokelewa (nakala ipo chini). Jopo la Mawakili linawahusisha Benedict Alex Ishabakaki, Peter Kibatala, Jebra Kambole na Jeremiah Mtobesya.

Kwa waliotaka kuchangia:

Napenda kuwashukuru watanzania wengi sana waliojitokeza (kunitafuta au kuwatafuta watu wangu wa karibu) kutaka kuchangia ili tulipe faini hiyo; niseme nimefarijika sana kuwa watu walikuwa tayari kufanya hivyo. Niwaombe kuwa msinichangie kulipa faini kwani tayari hili nimefanikiwa kulitekeleza na ndiyo maana nimeachiwa huru. Kwa wanaoona kuwa bado wanataka kunichangia kwa gharama nilizotumia, ninashukuru sana lakini naomba ijulikane kuwa tayari hili limekamilika; ukiamua kufanya hivyo – basi umefanya kwa kupenda na ninashukuru.

Kesi nyingine:

Kuna kesi nyingine yenye maudhui kama haya; kesi namba 458 ya mwaka 2016 ipo mbele ya Hakimu Huruma Shaidi na itaendelea Aprili 23, kutokana na janga la Corona wananchi hawaruhusiwi kusikiliza kesi hizi. Tutawapa update ya kitakachojiri siku hiyo kupitia hapa JF na katika kurasa zetu za mitandao ya kijamii. Soma Kesi namba 458 (Jamhuri v JamiiForums) yaahirishwa tena kwa kukosekana Shahidi. Mara ya mwisho kuwa na Shahidi ni Novemba 12, 2018 - JamiiForums

Kesi namba 457 ya mwaka 2016 iliisha baada ya hakimu Godfrey Mwambapa kuona hatukuwa na hatia hivyo kutuachia huru. Soma Kesi namba 457: Mahakama yasema Maxence Melo na Micke William hawana Kesi ya kujibu! Yawaachia huru - JamiiForums

Sababu za kesi hizi

Tulikuwa tukiandikiwa barua nyingi; hizi chini ni baadhi. Zote zilikuwa zikitaka data ambazo hata mbele ya Hakimu Simba wakati wa utetezi wangu nilimwambia HATUNA. Majibu ya wanasheria yalieleza wazi pia kuwa tulikuwa tayari kutoa ushirikiano wa kutosha endapo tungejua jinai ya wateja wetu; barua tulizojibu hazikupata majibu tena toka Polisi na badala yake nilijikuta nikitiwa mbaroni.

Mfano:

Kesi ya Oilcom – Mawakili wangu walibainisha kuwa kilichoandikwa ni Oilcom na wala haikuwa Oilcom (T) Ltd; na pia hao Oilcom hawakuja na ushahidi wa wao kuandikwa JF kwani printout yao ilikataliwa kama kielelezo. Hakimu Simba yeye anadai amejiridhisha kuwa kutakuwa kulikuwa na andishi hilo hata kama halikuletwa mahakamani. Hapa chini nimeambatanisha barua ya Polisi na majibu yetu (hakimu amesema tulichelewa kuwapa majibu hivyo amenitia hatiani).
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad