IMF: COVID-19 imelemaza uchumi wa dunia
0
April 04, 2020
Shirika la Fedha la Kimataifa IMF limesema kuwa janga la virusi vya corona limelemaza uchumi wa dunia na litasababisha mdodoro mkubwa wa uchumi wenye athari mbaya kushinda zile za mzozo wa kifedha wa mwaka 2008.
Akizungumza na waandishi habari kwa njia ya video mjini Washington, Mkurugenzi Mkuu wa IMF Kristalina Georgieva amezitaka nchi tajiri kuongeza juhudi za kuyasaidia mataifa yanayoendelea kukabiliana na athari za janga la corona.
Georgieva amesema IMF inashirikiana na Benki ya Dunia kuzirai nchi tajiri kusitisha kwa muda ukusanyaji madeni kutoka mataifa masikini hadi pale ulimwengu utafanikiwa kudhibiti kusambaa virusi vya corona.
Kiongozi huyo wa IMF amearifu kuwa ugonjwa wa COVID-19 umeathiri kwa sehemu kubwa uchumi na uwekezaji katika mataifa yanayoinukia akisema wawekezaji wameondoa mitaji ya hadi dola bilioni 90 kutoka mataifa hayo.
Hayo yanajiri wakati watu milioni moja na elfu 80 wameambukizwa virusi hatari vya corona kote duniani huku idadi ya waliokufa ikipanda na kufikia watu 57,474 kutokana na ugonjwa wa COVID-19.
Italia ndiyo imerikodi idadi kubwa ya watu waliokufa ambayo imefikia 14,681 ikifuatiwa na Uhispania, Marekani na Ufaransa.
Wakati virusi hivyo vikiendelea kusambaa, benki ya maendeleo barani Asia imeonya kuwa janga hilo litasababisha hasara ya hadi dola Trilioni 4.1 kwenye uchumi wa dunia kutokana na athari zake kwa mataifa tajiri.
Kadhalika mpango wa chakula wa Umoja wa Mataifa WFP umesema janga la Corona linatishia kusababisha upungufu wa chakula kwa mamilioni ya watu hususani barani Afrika.
Karibu nusu ya idadi ya watu duniani wameamriwa kubakia majumbani wakati mataifa ulimwenguni yanatanua juhudi za kupambana na virusi vya corona.
USA COVID-19 Schutzmasken in Kalifornien (picture-alliance/ZUMAPRESS/P. J. Heller)
Katika hatua nyingine serikali ya Marekani jana imetoa wito kwa raia wake kufunika pua na mdomo kwa kutumia barakoa wakiwa katika maeneo ya umma ili kujinga dhidi ya virusi vya Corona.
Wito huo umekuja wakati kuna wasiwasi kuwa virusi hivyo vilivyowakumba zaidi ya watu milioni moja duniani vinaweza kusambaa kupitia njia ya kawaida ya kupumua.
Rais Donald Trump amesema pendekezo la kuwahimiza raia wote milioni 330 wa Marekani kutumia barakoa pindi wakiwa maeneo ya wazi litakuwa la muda mfupi na lisilo la lazima.
Afisa wa afya wa ngazi ya juu nchini Marekani Jerome Adams amesema uamuzi huo umefikiwa kwa sababu watu wengi walio na virusi vya corona hawaoneshi dalili na kugeuka kitisho cha kuwaambukiza wengine.
Tangu kugundulika kwa virusi vya corona nchini China, wataalamu wa afya wamesema virusi hivyo husambaa kwa sehemu kubwa kupitia chafya na kikohozi.
Tags