Diwani wa Machame Magharibi kupitia Chama cha Mapinduzi Martin Munisi, amemkosoa Wakili Albert Msando kufuatia kauli yake ya kuwataka waandishi wa habari watoke na kutoa taarifa za Corona na kwamba Arusha hali ni mbaya ili hali hata yeye hakuwa amezingatia tahadhari yoyote.
Diwani Munisi ameyabainisha hayo, alipofanya mazungumzo maalum na EATV&EA Radio Digital, na kusema kuwa kauli alizozitoa Msando za kuwa Arusha hali ni mbaya zinaleta hofu kwa wananchi na kwamba kitendo cha kuwataka waandishi wawe mstari wa mbele kutoa taarifa za Corona ni makosa kwa sababu Serikali pekee ndiyo inatoa taarifa za mwenendo wa ugonjwa huo nchini.
"Wakili Msando alikuwa anazungumzia suala la Corona na kugawa vifaa ili hali hata yeye hakuwa amevaa Barakoa, na kile chumba kilikuwa ni kidogo na hakukuwa na tahadhari yoyote, na aliwataka waandishi kukusanya taarifa za Corona na ni wazi kabisa watu wanakufa kwa magonjwa mengine pia" amesema Diwani Munisi.
Aidha Diwani aliendelea kusema
"Sasa unapowaambia waandishi waende mtaani ina maana wakikuta mtu anazikwa waandike kafa kwa Corona na alisema hali ni mbaya ili hali na yeye anamiliki Baa ambayo inakusanya watu, ni vizuri tunapozungumzia masuala haya tuwe serious, inabidi tuzungumze mambo tunayoyaishi na uhalisia na kutoleta hofu na vitisho katika jamii".